Mwanza. Wakati Gwambina FC leo wakijiandaa kuwakabili Yanga katika mchezo wa kombe la FA, Kocha Msaidizi wa timu hiyo Athumani Bilali ‘Bilo’amesema wanajua presha kubwa waliyonayo wapinzani wao na kama wakiingia uwanjani na hasira basi watawapiga bao za kutosha.
Bilo alisema Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na hasira za kufanya vibaya Ligi Kuu hivyo wao wamejiandaa kikamilifu kuwakabili na wamejipanga kuondoka na ushindi katika pambano hilo.
Alisema presha ya Yanga katika mchezo huo itawasaidia wao kupata ushindi kwani wanajua kuwa wapinzani wao hao sasa wamebakiza matumaini ya ubingwa kwenye kombe hilo.
“Tunajua kuwa tunakutana na Yanga ambao wana hasira na presha kubwa ya kutaka kutufunga lakini hili sisi tunalifurahia kwa sababu tutaingia kwa tahadhari kubwa na tutawafunga tu,” alisema Bilo.
Bilo alisema wameshafanya maandalizi ya kutosha katika mchezo huo ambao kwao wanauchukulia kwa umakini mkubwa kwani wanataka kupata ushindi ambao utawafanya wasonge mbele katika mashindano hayo.
Alisema Yanga wasije kuwabeza kabisa katika mchezo huo kwani nao wana kikosi bora ambacho kimesheheni wachezaji wazoefu ambao walishawahi kucheza ligi kuu na wale Chipukizi.
Pia Soma
- Changalawe apigwa mabondia Tanzania wakosa tiketi ya Olimpiki Japan
- Ninja: Kombe la FA ni tiketi ya Yanga kimataifa
- Sven avunja mfupa uliomshinda Aussems Kombe la FA