YANGA wanagawa dozi huku wakisema timu yao inaendeshwa kisasa na habari mpya ni kwamba kuna mtaalamu mwingine ameshushwa kimyakimya na ameanza kazi na mshambuliaji, Bernard Morrison.
Wadhamini wa Yanga ambao ni Kamapuni ya GSM inayomilikiwa na Biilionea, Ghalib Mohamed ndio waliosimamia pia usajili wa timu hiyo, sasa wanasuka benchi la ufundi na juzi Jumapili wakamshusha mtaalamu wa tiba za viungo, Faried Cassiem.
Cassiem alitua juzi usiku na jana Jumatatu haraka alianza kazi katika kuwatibu wachezaji wa timu hiyo ambao ni majeruhi.
Akiwa mazoezini jana na kushuhudiwa na Mwanaspoti, Cassiem raia wa Afrika Kusini alianza kazi kwa kuangalia majeraha ya Morrison ambaye alikuwa akilalamika maumivu baada ya kumalizika kwa mechi ya juzi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Ujio wa Cassiem ni hatua ya kuyafanyia kazi mapendekezo ya kocha wao mpya, Luc Eymael ambaye alihitaji kuletewa mtu wa taaluma hiyo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said ameliambia Mwanaspoti kwamba kampuni yao bado inahitaji kuiona Yanga inabadilika na kuendeshwa kisasa na ujio wa Cassiem ni uthibitisho mwingine wa kukamilisha dhamira yao wakishirikiana na uongozi wa Yanga.
Pia Soma
- Balinya afunguka mazito Yanga
- Wachezaji 12 tishio Ligi kuu Tanzania Bara
- Polisi yamtolea macho Dilunga
“Kuna mambo lazima yaendeshwe kwa utaalamu hasa suala la matibabu, nikweli tumemleta Cassiem ambaye ni mtaalamu wa tiba za viungo hatua hii ni sisi GSM tukishirikiana na uongozi wa klabu ya Yanga kutekeleza mahitaji ya kocha mkuu,” alisema Said ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya mashindano ya timu hiyo.
Kabla ya kuja Yanga, Cassiem amefanya kazi katika klabu mbalimbali za Ligi Kuu Afrika Kusini zikiwemo Mamelodi Sundowns, Chips United na Ajax Capetown. Kwa kufanya hivyo, Yanga inaendana na falisafa za kuendesha klabu hiyo kisasa kama alivyotaka kocha wao mkuu.