Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bilionea Sheikh Jassim awapa masharti familia ya Glazer

Sheikh Jasmini Bilionea Sheikh Jassim awapa masharti familia ya Glazer

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uvumilivu umefika kikomo. Na sasa, mfanyabiashara tajiri wa Qatari, Sheikh Jassim amewapa masharti wamiliki wa Manchester United kuamua moja, wanauza timu yao au hawauzi.

Bilionea huyo ameiambia familia ya Glazer inayomiliki Man United: "Mniuzie hadi kufika Ijumaa…la najitoa."

Sheikh Jassim, mmoja wa wanafamilia ya kifalme katika nchi hiyo ya Guba, mapema wiki hii aliwasilisha ofa yake ya tano ya kutaka kuwa mmiliki wa jumla wa klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.

Lakini, kwenye mchakato huo, bilionea huyo wa Qatari atashindana na tajiri mkubwa kabisa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe katika harakati za kuimiliki Man United. Sheikh Jassim ameanza kuchoshwa na kupoteza imani juu ya familia ya Glazer kwenye ishu ya kufanya biashara ya kuiuza klabu hiyo na wasimamizi wa mchakato, Raine Group.

Na wakati ofa yao ya tano ikiwa mezani, Sheikh Jassim na kambi yake hawataendelea na jitihada za kutaka kuinunua Man United kama muda wao wa mwisho waliopanga kutaka jambo hilo limalizwe utakwisha.

Na kinachoelezwa ni kwamba tajiri huyo wa Qatari ametoa mwisho leo, Ijumaa - familia hiyo ya Glazer iamue, inamuuzia Man United au hawataki, akafanye shughuli zake nyingine.

Jambo hilo linaweza mauzo ya Man United kuangukia kwa tajiri Ratcliffe na kampuni yake ya Ineos - au familia ya Glazer ikalazimika kuingia kwenye sharti la bilionea wa Qatari na kufanya uamuzi hadi kufikia leo Ijumaa.

Sheikh Jassim anataka kuimiliki Man United kwa asilimia 100 tena kwa kulipa sehemu kubwa ya mkwanja wa kuinunua timu hiyo na kutamba kwamba atalipa pia madeni na kuifanya miamba hiyo ya Old Trafford isidaiwe.

Sheikh Jassim ameahidi pia pesa za ziada za kufanya usajili, kuboresha miundombinu na uwekezaji mwingine unaohitajika, kitu ambacho kwenye ofa ya Ratcliffe na kampuni yake ia Ineos hakuna mambo kama hayo.

Thamani ya Man United kwa sasa kwenye soko la hisa la New York ipo chini ya Pauni 2.5 bilioni na ofa ya tajiri huyo wa Qatari ni kubwa kuliko thamani ya klabu hiyo inavyoelezwa sokoni kwa sasa.

Ikiwa imepita miezi minne tangu alipopeleka ofa yake ya kwanza ya kuinunua Man United, huku dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi likitarajia kufunguliwa Jumatano ijayo, bilionea huyo wa Qatari ameamua kufanya uamuzi wa kibabe akiwaambia familia ya Glazer iamue ashachoka kucheleweshwa.

Sheikh Jassim amekuwa akiongoza na ofa zake mara zote alizoweka mezani mzigo wake, lakini bado hajafikia thamani ambayo familia ya Glazer wamepanga kuiuza klabu yao ya Ma United, Pauni 6 bilioni.

Ofa yake ya mwisho, iliyotoka mwezi uliopita inaripotiwa kuwa ya Pauni 5.5 bilioni. Lakini, ripoti nyingine zinadai kwamba Glazer wapo tayari kukubali ofa ya Ratcliffe na kampuni yake ya Ineos. Yeye anataka kuweka mzigo wa Pauni 3 bilioni na amiliki hisa kwa asilimia zaidi ya 50. Na kwenye mpango wake atawafanya wenyekiti wenza Joel na Avram Glazer kubaki kwenye klabu hiyo, licha ya kwamba ndugu zao wengine wanne watalipwa stahiki zao zote.

Kwa mpango wa Ratcliffe ni kwamba watakaoondoka Man United ni mkurugenzi mtendaji mkuu wa sasa Richard Arnold na wakurugenzi wengine. Ratcliffe anaamini kwa kuwa na hisa zijazozidi nusu itampa nafasi ya kuwa mwenye uamuzi mkubwa wa kuhusu mwenendo wa klabu.

Lakini, mashabiki wa Man United wanataka familia ya Glazer iondoke moja kwa moja kwenye timu hivyo, hivyo bila shaka shilingi yao wataweka upande wa Sheikh Jassim, hasa baada ya kuibuka kwamba ofa mpya ya Ratcliffe kutaka kuwabakiza wanandugu wote sita wa familia ya Glazer kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.

Chanzo: Mwanaspoti