Bilionea Todd Boehly amekuwa sehemu tamu ya tamthiliya ya Ligi Kuu England tangu alipokuwa mmiliki wa Chelsea, Mei 2022, alipotumia Pauni 1 bilioni kupata pointi kiduchu.
Boehly alifanya usajili wa pesa nyingi sana tangu dirisha la majira ya kiangazi 2022, aliposajili wakati kama Marc Cucurella, Raheem Sterling na Kalidou Koulibaly wakitua Stamford Bridge, lakini kocha aliyeletewa wachezaji hao, Thomas Tuchel alifutwa kazi Septemba.
Kisha akatumia Pauni 20 milioni kumchukua Kocha Graham Potter kutoka Brighton, hapo Chelsea ilionekana kama inaanza upya maisha, lakini matokeo ya hovyo yaliwafanya mabingwa hao wa Ulaya wa mwaka 2021 kuporomoka kwenye msimamo.
Baada ya kutumia mamilioni ya pesa kwenye dirisha la Januari 2023 aliwasajili wachezaji kama Enzo Fernandez na Mykhailo Mudryk, uvumilivu wa kubaki na Potter ukakoma Aprili na kocha huyo akafunguliwa mlango wa kutokea. Frank Lampard akarudishwa Chelsea na timu ikamaliza nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, nafasi ya hovyo zaidi kuwahi kushika kwenye ligi tangu msimu wa 1995-96.
Kocha Mauricio Pochettino akapewa kazi kwa msimu huu, huku Chelsea ikitumia zaidi ya Pauni 300 milioni kwenye dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi lililofungwa Ijumaa iliyopita.
Lakini, kipigo kutoka kwa West Ham United na Nottingham Forest kimempa kocha huyo wa zamani wa Tottenham, kwamba ana shughuli pevu ya kuirudisha Chelsea kwenye makali yake ya zamani.
Sawa bado mapema na msimu wa 2023-24 ndiyo kwanza utaanza, lakini Chelsea inahitaji kurudi kwenye ubora wake haraka hasa kutokana na pesa ilizotumia kusajili, kitu ambacho kitamfanya bilionea Boehly kutokuwa na uvumilivu kama timu yake itamaliza kwenye nafasi za katikati katika msimamo.
Mashabiki wa Chelsea hadi sasa hawaelewi nini shida kutokana na kile kinachoendelea kutokea kwenye timu yao katika kipindi cha miezi 16 iliyopita. Ukitazama msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma tangu Boehly aimiliki timu hiyo, Chelsea inatia huruma kutokana na pesa ilizotumia kusajili.
Kila timu hapa imecheza mechi 42, huku zikihusisha zile zilizokuwapo kwenye msimu wa 2022-23 na zinazoendelea msimu huu 2023-24. Cheki hapa pointi zilizovunwa kwenye Ligi Kuu England tangu tajiri Boehly alipotua Chelsea.
1. Man City – pointi 101, mabao +70 2. Arsenal – pointi 94, mabao +49 3. Man United – pointi 81, mabao +13 4. Liverpool – pointi 77, mabao +34 5. Newcastle United – pointi 74, mabao +35 6. Brighton – pointi 71, mabao +25 7. Tottenham – pointi 70, mabao +14 8. Aston Villa – pointi 67, mabao +4 9. Brentford – pointi 65, mabao +15 10. Fulham – pointi 56, mabao -4 11. Crystal Palace – pointi 52, mabao -8 12. West Ham – pointi 50, mabao -10 13. Chelsea – pointi 48, mabao -9 14. Wolves – pointi 44, mabao -31 15. Nottingham Forest – pointi 44, mabao -30 16. Bournemouth – pointi 41, mabao -38 17. Everton – pointi 37, mabao -29.