Ikicheza kwa mara ya kwanza katika uwanja wake wa nyumbani, Nelson Mandela leo Tanzania Prisons imekumbana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Biashara United.
Katika mchezo huo kila timu ilipambana kusaka matokeo mazuri ili kujinasua mkiani na wenyeji kujikuta ikiangukia kisago hicho na kuendelea kubaki nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi moja baada ya mechi nne.
Wenyeji walianza mpira kwa kasi kipindi cha kwanza lakini mashambulizi ya kulazimisha kwa dakika tofauti hazikuwa na manufaa yoyote kutokana na wapinzani kuzuia hatari zote.
Biashara United ambao hawakusafiri kwernda kucheza mechi ya marudiano Kombe la Shirikisho dhidi ya Alh Ahly Tripoli ya Libya walicheza kwa umakini na nidhamu, walijipatia bao la kuongoza dakika ya 44 kupitia kwa Ramadhan Chombo 'Redondo' aliyepiga shuti kufuatia mpira wa faulo na kudumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili licha ya mabadiliko kwa timu zote, Biashara United ndio ilifaidika zaidi baada ya kupata bao la pili likifungwa na Denis Nkane akimalizia vyema kwa kichwa krosi ya Atupele Green dakika ya 46.
Hata hivyo Biashara United ilionekana kuelewana zaidi kwa kutengeneza mashambulizi na dakika za nyongeza waliweza kujipatia bao la tatu kupitia kwa Awio Ambrose aliyetoka benchi na kuwaacha hoi Wajelajela hao.
Kwa matokeo hayo, Prison inaandika rekodi mbaya kwa kuwa miongoni mwa timu ambazo hazijaonja ushindi wowote kwenye mechi nne za Ligi Kuu na kumuweka katika wakati mgumu Kocha wake, Salum Mayanga.