Wanajeshi wa Mpakani, Timu ya Biashara United, neema imeanza kuwaangukia ndani ya kikosi chao baada ya kulamba mkataba mnono.
Mgodi wa dhahabu wa North Mara Gold Mine,leo umesaini mkataba na timu ya Biashara United Mara kuendelea kuifadhili timu hiyo.
Mkataba huo una thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 kwa muda wa miezi 9(msimu wa ligi).
Pamoja na udhamini huo North Mara Gold Mine wameahidi kutoa dola 45,000/= (zaidi ya shilingi milioni 100/-) kwa ajili kuisaidia timu hiyo itakaposhiriki katika mechi za kimataifa.
Mkataba huo umesainiwa mbele ya Katibu Tawala mkoa wa Mara Bw. Albert Gabriel Msovela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Ali Hapi ambaye amewataka wachezaji na benchi la ufundi kuhakikisha timu hiyo inamaliza ligi ikiwa katika nafasi 3 za juu.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Barrick North Gold Mine Apolinary Lyambiko amesema mgodi huo utaendelea kuwa karibu na timu hiyo ili kuendelea kuwa alama ya mkoa wa Mara sambamba na kuleta burudani ya kandanda mkoani hapa.