Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Biashara United wazidi kuididimiza Prisons

Biashara Mara 3 Biashara imeibuka na ushindi wa magoli 2-1

Tue, 15 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Timu ya Biashara United ya Mara imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya leo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.

Mchezo huo wa mzunguko wa pili Ligi Kuu ya NBC ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa timu hiyo tangu ilipohamishia hapo mechi zake ikianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Azam FC.

Biashara ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata mabao yake yakifungwa na mshambuliaji Deogratias Mafie katika dakika ya 26 na 33 akimalizia pasi kutoka Kwa Atupele Green na Ambrose Awiyo na kuitanguliza timu hiyo ikienda mapumziko kifua mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili Tanzania Prisons ilifanya mabadiliko ya wachezaji Adil Buha, Jeremiah Juma na Nurdin Chona nafasi zao zikichukuliwa na Mudathir Abdullah, Moses Kitandu na Ibrahim Abraham ambao walileta uhai mkubwa kwenye timu wakiongeza mashambulizi  na kupunguza hatari langoni mwao.

Mabadiliko hayo yalileta manufaa kwa maafande hao ambao walipata bao mnamo dakika ya 68 lilifungwa na Ezekia Mwashilindi kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa na kujaa wavuni.

Mabao hayo yalidumu hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Biashara wakiibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 2-1 na kuendeleza ubabe mbele ya maafande hao bada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza kushinda mabao 3-0 ugenini katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.

Ushindi huo unaifanya Biashara United kufikisha pointi 19 na kusalia kwenye nafasi ya 14 huku Prisons ikibaki na pointi zake 13 kwenye nafasi ya 16 huku timu hizo zikicheza michezo 18 kila moja.

Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Kazumba amesema bado wanayo nafasi ya kujikwamua kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi kwa kushinda michezo yao iliyobaki ikiwemo sita ya nyumbani huku akiahidi kuyatumia mapumziko ya wiki moja kupisha mechiza timu ya taifa kurekebisha makosa.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz