Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Besiktas yampigia hesabu Mtanzania

Mbongo Pc Besiktas yampigia hesabu Mtanzania

Mon, 8 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nyota imeng’aa kwa kiungo mshambuliaji wa Kitanzania, Shafii Omary Lumambo ambaye anaichezea Tuzlaspor ya Uturuki kiasi cha kuziingiza vitani klabu mbalimbali kubwa nchini humo ikiwemo Besiktas.

Mchezaji huyo mwenye miaka 19, ni miongoni mwa wachezaji ambao wamefanya makubwa katika ligi ya vijana, ndani ya michezo 22, amehusika katika mabao 24 kwa kufunga 13 huku akitoa asisti 11 ambazo zimelisaidia chama lake kutinga hatua ya mchujo (play-offs) ambayo itahusisha wababe kutoka makundi mengine.

Taarifa kutoka Uturuki zinasema Besiktas ndio wanaoongoza vita hiyo huku ikielezwa maskauti wake wanaendelea kumfuatilia kijana huyo wa Kitanzania katika hatua inayofuata kitaifa ambayo itahusisha jumla ya timu 16.

Kwa mujibu wa gazeti la Fanatik la nchini humo, Shafii aliandikwa mwanzoni mwaka huu kuwa ni miongoni mwa wachezaji wa kutazamwa katika ligi hiyo chini ya umri wa miaka 19 ambayo alianza kucheza akiwa na miaka 18.

Miongoni mwa wanahabari wa gazeti hilo ambaye jina lake hakutaka kuwekwa wazi amemuelezea, Shafii kwa kusema ni kijana mwenye kipaji kikubwa ambaye anaweza kupata nafasi haraka ya kucheza ngazi ya juu ya soka nchini humo kutokana na kile ambacho anafanya katika ligi ya vijana.

“Nilipomwona kwa mara ya kwanza niligundua kuwa ni kijana mwenye kipaji lakini nilijipa muda wa kuendelea kumtazama na amethibitisha hilo kwa mchezaji ambaye sio mshambuliaji wa mwisho halafu anafunga mabao 13 na kutoa asisti 11 hii inaonyesha namna gani ana kitu kikubwa ndani yake,” anasema na kuongeza;

“Sikushangaa nilipoona maskauti ya Besiktas wakimfuatilia, siku moja nilimuuliza mmoja na kugundua kuwa wapo ‘serious’ naye na pengine lolote linaweza kutokea mwisho wa msimu, anaonekana kuwa na kitu kikubwa, tusubiri tuone.”

Kwa upande wake, Shafii ambaye anafurahia maisha ya soka la Uturuki, anatambua kuwa anafuatiliwa na maskauti mbalimbali hivyo amekuwa akijitahidi kufanya vizuri katika kila mchezo ambao amekuwa akipata nafasi.

“Najua kuwa hii ndio njia kwangu ya kufikia malengo yangu, nimekua nikimwomba Mungu huku nikipambana kwa uwezo wangu wote ili kufanya vizuri, katika kila mechi nimekuwa nikikaa chini na kocha kwa ajili ya kujifunza zaidi na yeye hunipa tathimini yangu, wapi nilifanya vizuri na wapi nilifanya vibaya ili kuboresha katika mchezo unaofuata,” anasema kinda huyo.

Licha ya kuwa mchezaji wa kikosi B cha Tuzlaspor, Shafii amekuwa akipata nafasi pia ya kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha wakubwa ambacho kinashiriki katika ligi daraja la kwanza nchini humo ambayo ni maarufu kama TFF First League. Ni ligi ya pili kwa ukubwa kwenye soka la Uturuki.

Kocha wa Tuzlaspor, Bekir Irtegun amewahi kumuongelea Shafii kwa kusema ni vizuri kwa umri wake kutumika katika ligi ya vijana ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kukua zaidi kiushindani.

“Isingekuwa sawa kuharakisha kumtumia katika kikosi chetu cha kwanza, ni mchezaji mzuri lakini alitakiwa kuendelea kukua katika timu zetu za vijana kabla ya kuanza kumtumia, kwa sasa anaonekana kuwa tayari na amekuwa akijituma hata katika mazoezi ambayo tumekuwa tukifanya naye,” anasema.

Taarifa za Shafii kuhusishwa na Besiktas zimepokewa vizuri na taasisi ya kuvumbua na kuendeleza vipaji vya vijana nchini (AYE) ambayo ilimtoa kijana huyo kwa kusema wanamtakia kila la kheri huku wakiamini kufanikiwa kwake ni kuendelea kufungua milango kwa wachezaji wengine ambao wapo mtaani.

Mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Muyimba Gerald anasema alivyopokea taarifa hizo, alifanya mawasiliano na wadau wao ambao wapo Uturuki.

“Kwetu ni habari njema, tunaamini kwa uwezo wa kijana, Tuzlaspor itapokea ofa nyingi na sisi tumekuwa tukimweleza afanye kazi, aache miguu yake iongee kila kitu kitakuwa sawa, shauku ya Shafii ni kucheza soka katika levo za juu, anajua kuwa Uturuki kwake ni njia na kama hivyo vyombo vya habari vimeanza kuongelea ni hatua nzuri na kubwa kwake,” anasema.

Gerald anasema kupitia Shafii, uongozi wa AYE umekuwa na kiu ya kuingia mtaani na kuendelea kuibua vipaji vya vijana wengine na kuwaendeleza katika klabu mbalimbali ndani na nje ya Afrika kwa ajili ya kutimiza ndoto zao.

Chanzo: Mwanaspoti