Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benzema kwenye tabia za asilia ya Wafaransa

Benzema Ahusishwa Na Ugaidi Benzema kwenye tabia za asilia ya Wafaransa

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ukifuatilia kwa karibu moja ya habari zinazozidi kupamba moto kila wiki ni kile kinachoendelea kati ya Karim Benzema na Al Ittihad ambapo kwa sasa staa huyo ameachwa nje ya kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa ya Asia.

Staa huyu ameachwa kutokana na kile kinachoendelea kati yake na kocha wa timu hiyo Marcelo Gallardo baada ya Benzema kuchelewa kwa siku zisizopungua tano kutoka kwenye mapumziko waliyopewa Januari kabla ya kurejea kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu nchini Saudi Arabia.

Benzema ambaye alienda kupumzika nchini Maurtius alipokuwa huko hakuwa anapokea simu na muda mwingine simu yake hata haikuita kabisa.

Aliporejea alisimamishwa na alipojaribu kwenda mazoezini kocha wake Gallardo alimwambia aondoke kisha baada ya hapo akapewa maelekezo ya kufanya mazoezi peke yake.

Ilipofika Jumanne ya wiki iliyopita alionekana akifanya mazoezi na wachezaji waliokuwa wanarejea kutoka kwenye majeraha, hadi sasa hajarudishwa kwenye kikosi na inaelezwa kwamba ameondolewa kwenye kikosi kitakachocheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Asia.

Benzema amezaliwa pale jijini Lyon nchini Ufaransa, amekulia hapo pia.

Kwa mujibu wa tovuti mbali mbali moja ya sifa kubwa za mji huu ni kuwepo kwa wizi wa aina mbalimbali.

Kumekuwa na tabia ya watu kuibiwa kwenye usafiri wa jamii, wengine wanaibiwa mitaani na inadaiwa kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uhalifu ndio umezidi kupamba moto.

Hushangazi sana kumuona staa huyu akiwa kwenye mikasa kama hii, kutokana na tabia za mastaa mbali mbali kutokea nchini humo.

Mwaka 2015, Benzema alidaiwa kushirikiana na baadhi ya wahuni kutoka nchini Ufaransa kwa ajili ya kumtishia mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Mathieu Valbuena alipe pesa la sivyo wangeachia video zake za faragha akiwa na mwenza wake.

Licha ya kwamba Benzema yeye alimfuata Valbuena kama mshauri lakini mahakama ilimkuta na hatia na kumuamuru alipe fidia ya Pauni 63,000.

Kiasi cha pesa ambacho majambazi hao walikuwa wakidaiwa kukihitaji ili wasivujishe video hizo kilikuwa hakifikii hata Euro 300,000 ikiwa na maana ya kwamba Benzema angeweza kupata hata kwenye mshahara wake wa wiki mbili lakini bado alikutwa na hatia ya kufanya jambo hilo. Kwanini? ndivyo walivyo yeye na washkaji zake.

Mkasa huu ulisababisha aondolewe kwenye timu ya taifa ya Ufaransa ambapo hakuwepo pia kwenye kikosi kilichochukua ubingwa wa fainali hizo mwaka 2018 kule Urusi.

Man United ilibahatika kuwa na mmoja kati ya washambuliaji bora duniani, Eric Cantona, licha ya kucheza chini ya Sir Alex Ferguson aliyesifika kwa kuweka sawa nidhamu za wachezaji lakini jamaa bado alikuwa mtukutu sana. Moja ya matukio yanayokumbukwa sana kutoka kwake ilikuwa ni lile la mwaka 1997 la kumpiga teke la kung-fu shabiki wa Crystal Palace kwenye mchezo dhidi ya timu hiyo.

Mwaka 2022, kiungo wa West Ham, Kourt Zouma alihukumiwa kufanya huduma za kijamii kwa saa 180 baada ya kusambaa kwa video yake iliyokuwa inaonyesha kwamba anampiga paka.

Pia alikatwa mshahara. Basi jamaa ndio maisha yao hayo. Ukitafuta wachezaji wasiokuwa na drama nje ya uwanja ambao wanatokea Ufaransa upata wachache sana, zaidi watu wengi huangukia kwa N’Golo Kante.

Na haya yamekuwa hayafanyiki kwenye mpira wa miguu peke yake bali utukutu wa wana michezo wa Ufaransa upo pia sehemu nyingine.

Mwaka 2017, Marseille ilimvunjia mkataba beki wa zamani wa Manchester United, Patrice Evra baada ya kumpiga shabiki wa timu yao wenyewe wakati wa mazoezi ya kuweka miili sawa kabla ya mchezo wa Europa League dhidi ya Vitoria Guimaraes.

Mbali ya kuvunjiwa mkataba pia alipigwa faini ya Euro 10,000. Mwaka 2022, wakati Patrick Vieira akiwa anaifundisha Crystal Palace aliwahi kuingia matatani baada ya kusambaa kwa video yake akiwa anapigana na mashabiki wa Everton waliovamia uwanjani baada ya mchezo wao dhidi ya timu hiyo. Ni ngumu sana kuona ama kusikia mambo haya kwa makocha wakubwa kama Vieira.

Mwaka 2010 kwenye Kombe la Dunia kule nchini Afrika ya Kusini Nikolas Anelka alirudishwa nchini Ufaransa mapema baada ya kugombana na kocha wa wakati huo wa Ufaransa Raymond Domenech na haikuwa peke yake tu kwani baadae Patrice Evra, Franck Ribery, Eric Abidal na Jeremy Toulalan pia walidaiwa kuitwa kwenye kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka la Ufaransa kujibu juu ya kukataa kwao kufanya mazoezi na timu wakati wa mashindano hayo.

Hiyo ilikuwa ni michuano ta Kombe la Dunia na mastaa hawa bado wakagoma kufanya mazoezi.

Kuna wakati wachambuzi walimsema sana Paul Pogba kwa kitendo cha kuwa anaitishia Man United kwamba anaweza akaondoka, Jose Mourinho wakati anaondoka kama kocha wa timu hiyo mwaka 2018 aliwahi kusema kwamba Paul Pogba ni kirusi kwenye timu, kiungo huyu pia ni Mfaransa.

Mwaka 2023, mchezaji wa tenisi kutoka nchini humo Hugo Gaston alitozwa faini ya Euro 144,000 kwa kufanya vitendo visivyokuwa vya kiuanamichezo.

Ukiondoa haya kumekuwa na matukio mengi ya aina hii kutoka kwa wachezaji wenye uraia wa Ufaransa. Inawwezekana ikawa ndio hulka yao, lakini hilo linaweza kuchangiwa na mambo mengi pengine hata mazingira ambayo wamekulia. Hivyo Benzema ni kama anaenzi tu washkaji zake.

TAKWIMU ZAKE

Kwenye maisha ya soka hadi sasa, Benzema amechukua tuzo ya Ballon d’Or mara moja, mchezaji bora wa bara la Ulaya mara moja, Mchezaji Bora wa Ufaransa mara nne na akawa mfungaji bora wa michuano mbali mbali mara sita. Pia kiujumla amechukua mataji 36.

Chanzo: Mwanaspoti