Pengine sasa nafasi za Wanasimba zitatulia baada ya ujio wa kocha Abdelhak Benchikha kutoka Algeria ambaye msimu uliopita aliipa USM Alger taji la Kombe la Shirikisho Afrika na baadaye akaipatia lile la CAF Super Cup kwa kuzifunga Yanga na Al Ahly zinazovaana kesho kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni mtu mwenye ubishi wa asili tu ndiye anayeweza kubeza ubora na heshima ya Benchikha katika kazi ya ukocha wa soka hapa Afrika na wasifu wake unatoa majibu tosha hivyo iko wazi Simba wamepata bonge la kocha.
Na ilikuwa lazima Simba ipate kocha wa daraja lake kutokana na yale waliyoyapitia katika siku za hivi karibuni hal’kadhalika ugumu na mahitaji ambayo inayo kwenye mashindano inayoshiriki ya ndani na yale ya kimataifa ambayo haijafanya vizuri kwa misimu miwili iliyopita.
Ushauri wangu kwa Simba ni kutoweka matarajio makubwa ya muda mfupi kwa Benchikha kwamba airudishe timu yao kwa haraka kwenye mstari katika ligi ya ndani pamoja na mashindano ya kimataifa kisa tu huko alikotoka alikuwa amefanya vizuri.
Inawezekana hilo likatokea, lakini wasiliwekee matarajio makubwa kwa sababu, kocha anakikuta kikosi ambacho yeye hakuhusika katika usajili, hivyo atahitaji muda wa kumfahamu mchezaji mmoja mmoja na kuutathmini ubora wake kuona kama anafaa au hafai katika kile ambacho anataka kukiingiza ndani ya timu.
Anawakuta wachezaji ambao wengi wao wanaonekana kuporomoka viwango na pia wamepoteza hali ya kujiamini, hali ambayo haitochukua muda mfupi kuibadilisha kwani kila mmoja ameumbwa na uwezo wake wa kurudi katika hali ya kawaida baada ya kupitia kipindi cha kupoteza uwezo wa kujiamini.
Pia juhudi pekee za kocha hazitoshi kuifanya timu ifanikiwe na badala yake anahitaji ushirikiano wa pamoja wa maofisa wenzake wa benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba na sio kuachiwa mzigo peke yake jambo ambalo hatoliweza na mwisho wa siku akaishia kubwaga manyanga na kuondoka zake.
Pia hatakiwi kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake na apewe uhuru mkubwa wa kufanya kile ambacho anakiona ni sahihi kwa ajili ya timu jambo ambalo litatoa uhalali wa kumuadhibu ikiwa atashindwa kuzalisha matunda.