Shabiki kindakindaki wa Klabu ya Simba, anayefahamika kwa jina la Mchome Mapovu amesema kuwa Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Abdelhak Benchikha sio kocha mkubwa kwani ameshindwa kuibadilisha timu yake ili iweze kucheza vizuri na kupata matokeo kama yalivyo matarajio ya wengi ndani ya timu hiyo.
Simba atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Jwaneng ya Botswana wakiwania kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika, mchezo utakaopigwa jumamosi Februari 3, 2024 katika Dimba la Mkapa.
“Benchikha sio kocha mkubwa ila ana CV kubwa, makocha wakubwa ni kama kina Master Gamondi, Nasreddine Nabi, yani anakuja kocha ambaye ni mkubwa lakini hana CV kubwa, anakuja anaonyesha kitu lakini Benchikha ameshindwa kuibadilisha timu.
“Kocha ana wachezaji kila siku ndiye anayewafundisha lakini uwanjani ana kazi ya kulalamika tu. Benchikha ukimfuatilia kwenye mechi kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya 90 yeye analalamika tu, anatupa mikono muda wote, mchezaji akimpa pasi mwenzake, yeye kocha analalamika.
“Huyu kocha anatengeneza mazingira ili waonekane wanachokifanya wachezaji sio kile anachowafundisha mazoezini. Kama timu imemshinda aiache aondoke.
“Kabla ya kuja Simba tayari alikuwa anawajua wachezaji wa Simba na mfumo wa timu ndiyo maana akakubali kuja kuifundisha, anavyoanza kulalamika sisi anatuboa,” amesema Mchome Mapovu.