Kocha Mkuu wa Simba, Mualgeria Abdelhak Benchikha, ameanza kuonesha makucha yake kwa kusema hatoangalia ukubwa wa jina la mchezaji au kipenzi cha nani, zaidi ya kutaka kuona kiwango bora na kupambania klabu hiyo kufikia malengo.
Benchikha tayari amewasili huku akiambatana na wasaidizi wake wawili, Farid Zemiti ambaye atakuwa kocha msaidizi na Kamal Boudjenane wa viungo.
Kocha huyo tayari yuko nchini kuchukuwa nafasi ya Robertinho Oliveira na wenzake kuendelea kukinoa kikosi cha ‘Wekundu wa Msimbazi’ hao wakijiandaa na mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Benchikha amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kukinoa kikosi hicho kuhakikisha kinafikia malengo yao ya kutwaa ubingwa wa ligi ya ndani na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza nasi, Benchikha alisema malengo yao ni kufanya vizuri, hivyo lazima kila mchezaji anatakiwa kupambana na si kujiona mkubwa ndani ya timu kwa sababu lengo lake kubwa ni kuifanya timu hiyo kupata ushindi uwanjani na kutwaa mataji mbalimbali ya ligi ya ndani na kufikia malengo katika michuano ya kimataifa.
Alisema ili timu kupata mafanikio, lazima kuwapo kwa mshikamano baina ya timu, viongozi na mashabiki kuisapoti timu yao. “Ninafuraha kuwa sehemu ya familia ya Simba, ni timu kubwa Afrika, ni furaha kuwapo sehemu ya historia ya hapa.
Tupo pamoja na mashabiki wa Simba na wanatakiwa kuwa imara kuvuka katika hili na tupo tayari kuwapa kiwango bora uwanjani.
“Kuna vingi navijua, nimekuja na mikakati yake na nitapata nafasi ya kuona wachezaji wangu na kuangalia yupi ananifaa au hanifai, suala la mashindano ninaimani nitafanikiwa kufanya vizuri kwa sababu mimi ni mpambanaji,” alisema Benchikha.
Aliongeza kuwa anaimani atawafurahisha mashabiki kwa kutengeneza Simba mpya na imara, kikubwa anahitaji sapoti na ushirikiano mkubwa kutoka kwao na kufanikisha kile ambacho wanakitarajia.
Kocha huyo alisema amekuja kwa malengo ya kufanikiwa kwa Klabu ya Simba kama ilivyo kwa klabu alizotoka kubwa zaidi ni ushirikiano mkubwa. Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula, alisema wanatamatisha shauku ya mashabiki kumpata mwalimu na kwamba walipokea wasifu nyingi kutoka kwa makocha mbalimbali, lakini walikuwa na kipindi kigumu kupata kocha mzuri kama ilivyo kwa Benchikha.
“Benchikha atakuwa Simba, atamalizia msimu huu na msimu ujao, mashabiki wanatakiwa kuwa watulivu kwa sababu ni kocha mpya, viongozi tumempa uhuru wa kufanya kazi na hatuna utaratibu wa kumpangia kocha kikosi nani acheze na asicheze,” alisema Kajula.
Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, ametamba kuwa wamepata kocha mzuri, Benchikha, ambaye yuko katika orodha ya makocha watano bora wanaowania tuzo ya kocha bora Afrika.
Alisema ni kocha mwenye uzoefu mkubwa, hivyo wanaimani ya kufikia malengo yao kwa sababu ya falsafa ya Benchikha kutaka ushindi na mafanikio katika klabu ambayo anaifundisha.
“Wakati tuko kwenye mazungumzo alituomba tumweleza mipango yetu ya sasa na ijayo, tukafanya hivyo na kukubaliana nasi na amekuja na wasaidizi wake akiwa na kocha msaidizi na viungo.
“Matarajio yetu makubwa kulingana na kocha tuliyempata, huyo kazi ataifanya kikubwa ni kumpa ushirikiano na muda. Ni kocha mwenye msimamo kweli kweli, tutampa uhuru katika kazi yake na wachezaji wamemwahidi kumpa ushirikiano mkubwa,” alisema Ahmed.
Alisisitiza kuwa benchi la ufundi halitaingiliwa kwenye majukumu na maamuzi yao, na juzi alitembelea kambi ya mazoezi na leo atakuwa na kibarua cha kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja na kesho, Alhamisi kuanza kazi rasmi.
“Ujio wa Benchikha vilio sasa basi, vimefika kikomo, hawa watu wamekuja kutufuta machozi, amekuja kutupatia maisha mapya ndani ya Simba.
“Suala la usajili amekabidhiwa kocha huyo baada ya kuona kikosi chake ataeleza ni wapi afanye maboresho kwa kuongezea watu, hilo linakuja baada ya kuona timu yake,” alisema Meneja huyo.