Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa, ushindi wanaoupata timu hiyo kwa sasa wa kumpa sifa ni kocha wao, Angel Miguel Gamondi.
Kamwe amesema hayo baada ya kumaliza deni lao na timu ya Ihefu FC ambapo jana Jumatatu, Machi 11, 2024, waliifunga mabao 5-0 katika Dimba la Azam Complex huku akiongeza kuwa, kulikuwa hakuna haja ya Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha kuikimbia timu yake na kwenda kufanya mafunzo ya wiki moja nyumbani kwao Algeria.
“Matokeo mazuri tunayoyapata kwenye kikosi chetu ni kutokana na kazi nzuri anayoifanya kocha wetu Master Gamondi. Kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji, sifa kubwa ziende kwa Master Gamondi na si mtu mwingine.
“Sijui kwa nini watu wamepoteza gharama kubwa kumsafirisha mtu kwenda shule mbali huko. Wangekuja tu Avic Town pale nauli ni Tsh 400 au Tsh 600, kuna kozi pale, Master Gamondi amempa shule pale ya siku tano au sita, akarudi kazini kwae. Sasa amesafiri ndege tatu kwenda kutafuta kozi ambayo pale Avic Town angeipata bure.
“Sisi tungempa na chakula cha asubuhi, mchana na jioni awe anasoma tu kwamba hivi ndivyo jisni ya kumfunga Prisons na hii ndiyo namna ya kumkaba Mbangula. Hiyo session angeipata pale, mambo haya ya kishingo yasingetokea. Sasa mtu kapigwa chuma mbili kachanganyikiwa, kakimbia. Angekuja kwa Gamondi angefundishwa akaelwa,” amesema Ally Kamwe.