Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha anaitaka fainali ya CAFCL

Benchikha Mashabiki  U2.jpeg Benchikha anaitaka fainali ya CAFCL

Fri, 1 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huko Simba kumekucha. Wameondoka leo kwenda Botswana kwa majukumu ya kimataifa, lakini kocha ametikisa kwelikweli huko kambini juzi jioni.

Kocha mpya, Abdelhak Benchikha alipokutana na wachezaji kwa mara ya kwanza amewasisitiza, hakuna aliye salama kwa sasa, huku akitaja kipaumbele chake.

Kocha huyo raia wa Algeria alichofanya cha kwanza kwenye kikao ni kumsimamisha mchezaji mmoja baada ya mwingine na kumtaka ajieleze mwenyewe, yeye ni nani, umri, anacheza nafasi ipi na amepata mafanikio gani msimu huu akimaanisha kama ni straika umefunga na kuasisti mabao mangapi.

Mastaa wote wakasimama wakajieleza, akawa anawasikiliza na kunukuu kwenye kitabu chake akisaidiwa na wasaidizi wake. Benchikha anayetajwa kuwa mmoja kati ya makocha wasiotaka masihara kwenye kazi, baada ya utambulisho huo wa mastaa wakapanda gari wakaelekea mazoezini kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena.

Kocha huyo aliyepewa na Simba mkataba wa mwaka mmoja na nusu, akiwa na kazi ya kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Federation na kutimiza lengo la kufika nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kinasema kuwa baada ya kocha huyo kufika kambini alionana na mchezaji mmoja mmoja, ambapo baadhi ya maswali ambayo aliwauliza ni umri, aina ya majeraha ambayo amekuwa anakutana nayo na takwimu zake za msimu huu.

Alikwenda mbali zaidi kwa kuwaambia, hakuna mwenye uhakika wa kucheza hata kama huko nyuma alikuwa bora kwani anataka kuona sasa mazoezini na si mambo ya historia.

“Kocha alionana na wachezaji kila mmoja na kuzungumza nao, aliongea mambo mengi lakini kubwa aliwataka wapambane kuanzia kwenye mechi ijayo dhidi ya Jwaneng Galaxy kwa kuwa ndiyo mchezo wa kwanza atakuwa anawatazama.

“Aliwaambia wachezaji kuwa hatawaangalia kwa rekodi za nyuma, hata kama mchezaji alikuwa bora huko nyuma kwa sasa hilo hawezi kuliangalia bali atakuwa anaangalia kuanzia sasa mchezaji anafanya nini yeye akiwa ndiye kocha,” kilisema chanzo chetu ndani ya kikao hicho kilichokuwa na utulivu mkubwa, huku wachezaji wengi wakiwa wamekunja mikononi kwa umakini.

Kocha huyo amesema atajitahidi kadri ya uwezo wake kuhakikisha kila mmoja anakuwa bora kwenye nafasi yake na nyingine am-bayo atatakiwa kucheza uwanjani na ikishindikana ataomba uongozi umpe mchezaji mwingine.

“Aliwaambia wachezaji kuwa hatari iliyopo ni kwamba yupo karibu na kipindi cha usajili na hivyo kila mmoja anatakiwa kuonye-sha ubora wake kwa muda mchache uliobaki na kama ikishindikana ataingia kwenye usajili Januari, nafikiri jambo zuri ni kwa kuwa amekuwa mkweli kwa wachezaji na anaonekana hataki masihara.”

FAINALI YA AFRIKA Mbali na hayo, chanzo hicho kimesema, kocha huyo amewaambia viongozi wa baadhi ya watu wa benchi la ufundi kuwa anataka kuhakikisha anafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kocha amesema anachofikiri yeye ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na ikiwezekana ku-fika fainali, lakini ikishindikana huko basi atwae ubingwa wa Ligi Kuu Bara.”

Hii inaweza kuwa sawa na jinsi ambavyo kocha huyo alifanya akiwa na USM Algier alipotwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho mbele ya Yanga, lakini kwenye Ligi Kuu ya Algeria timu yake ilimaliza kwenye nafasi ya 11 kati ya timu 16.

Simba inayoshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu nyuma ya Yanga na Azam, ilitarajiwa kuondoka alifajiri kwenda Botswana kwa ajili ya mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy baada ya mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Mkapa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Baada ya mchezo huo, Simba itasafiri tena hadi Morocco kuvaana na Wydad Casablanca.

Mchambuzi wa Mwanaspoti, Edo Kumwembe alisema, kama kocha huyo anataka kufanya vizuri ndani ya Simba ni kuhakikisha ubora wa wachezaji unakuwa juu haswa kwa Clatous Chama mwenye rekodi nzuri ndani ya kikosi hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live