Tukutane Kwa Mkapa. Ndio kituo kinachofuata kwa Simba baada ya jana usiku kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca kwa kuchapwa bao 1-0, ugenini kwenye Uwanja wa Marrakech, Morocco.
Simba sasa itaisubiri Wydad katika mechi ya marudiano itakayochezwa Uwanja wa Mkapa, Desemba 19.
Bao hilo la Zakaria Draoui la dakika za jioni, Simba sasa imeshuka hadi mkiani ikiwa na pointi mbili huku Wydad ambayo haikuonja ushindi wowote kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipanda hadi nafasi ya tatu na pointi zao tatu. Asec Mimosas ndiyo inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Jwaneng wenye pointi nne.
Simba bado ina nafasi ya kutinga robo fainali endapo itashinda mechi zao tatu na mbili nyumbani na moja ugenini.
Baada ya Wydad, Simba itaifuata Asec kabla ya kurudi kumaliza na Jwaneng Kwa Mkapa mwakani.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Simba ilicheza vizuri dakika 45 za kwanza na kama utamsaka mchezaji bora kwao basi ni kipa Ayoub Lakreb aliyefanya kazi kubwa kuokoa mkwaju wa penalti dakika ya 39 iliyopigwa na kiungo na nahodha wa Wydad, Yahya Jabrane.
Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji Kibu Denis kumwangusha winga wa Wydad, Saif Bouhra wakati akiingia ndani ya eneo la hatari.
Kipindi hicho cha kwanza Simba ilionekana kucheza kwa umakini mkubwa wakitengeneza nafasi huku wakionyesha kubadilika kwa kuwa na kasi wakielekea lango la wenyeji wao.
Simba ilikaribia kupata bao dakika ya 44 kupitia Sadio Kanoute lakini akashindwa kuunganisha mpira ulitokana na tik tak ya mshambuliaji wake Jean Baleke aliyepokea krosi ya beki Shomari Kapombe.
Kipindi cha pili Wydad walibadilika na kuishambulia Simba huku wekundu hao nao wakijibu mapigo lakini hakukuwa na utulivu kwa washambuliaji wake kutumia nafasi.
Hicho kinakuwa kipigo cha kwanza kwa kocha Abdelhak Benchikha tangu apokee ajira hiyo na sasa watarudi nyumbani Desemba 19 kurudiana na Waarabu hao.
DK 360 SIMBA
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha ana dakika 360 za kuonyesha ubabe wake kwenye Ligi Kuu Bara kabla ya mwaka 2023 haujafikia tamati kuupisha 2024.
Simba na Wydad zilikuwa zikipepetana kwenye mechi ya Kundi B, likiwa ni pambano la pili kwa Benchikha tangu alipotua Msimbazi kutoka Algeria na timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki ijayo jijini Dar es Salaam, lakini kabla ya mechi hiyo ya marudiano, hapo kati kutapigwa mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo utakuwa ni wa kwanza kwa Benchikha katika Ligi Kuu tangu aliposainishwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu na utakuwa ni dhidi ya Kagera Sugar na utapigwa wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kisha ndipo itarudiana na Wydad Jumatano ya wiki ijayo.
Baada ya hapo kocha Benchikha atakuwa na dakika nyingine 270 za kumalizana na mechi tatu za ligi kufungia mwaka 2023, akianza na KMC ambao utapigwa Desemba 23 Uwanja wa Uhuru, Wana Kinondoni wakiwa ndio wenyeji, kisha Simba itasafiri mikoa ya Kigoma na Tabora kucheza mechi mbili za viporo.
Simba itaanzia Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma kuvaana na Mashujaa siku ya Boxing Day na siku chache tatu baadae itahamia Tabora kumalizana na Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Hata hivyo, uwanja huo kwa sasa umefungiwa na Tabora kucheza mechi zake za nyumbani, Jamhuri Dodoma, japo wamiliki wake waliwahakikishia mashabiki mchezo huo wa Simba utapigwa Ali Hassan Mwinyi kwa vile watakuwa wameshakamilisha ukarabati waliotakiwa kuufanya.
Mechi hizo nne za Ligi Kuu kabla ya kuuaga mwaka 2023 ni kama kamtego flani kwa Benchikha kwenye ligi kwani itakuwa ni mara ya kwanza kwake kuiongoza timu hiyo kwenye mechi hizo, lakini akiwa na kazi ya kuvuna jumla ya pointi 12 zitakazoifanya timu ikae pazuri kabla ya kuisubiri Azam FC inayoongoza msimamo.
Simba na Azam zinatarajiwa kuumana Januari Mosi, ikiwa ni siku ya kwanza ya Mwaka Mpya wa 2024, huku rekodi zikionyesha kwa msimu uliopita Wanalambalamba wakitambia Mnyama kwa kuvuna pointi nne kati ya sita kwa kushinda mchezo mmoja kwa bao 1-0 kisha kutoka sare ya 1-1 na hata kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), Wekundu walilala tena kwa mabao 2-1, huku mabao matatu katika mechi hizo tatu yakifungwa na Prince Dube.
Dube kwa msimu huu ameshafunga mabao matano katika Ligi Kuu Bara akiwa nyuma ya Feisal Salum mwenye saba akilingana na Jean Baleke wa Simba pamoja na Maxi Nzengeli na Stephane Aziz KI wote wa Yanga.
Mashabiki wa Simba wana kiu ya kutaka kuona Benchikha akiwarudishia furaha kwenye Ligi Kuu baada ya mtangulizi wake, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuondoka akiwaachia simanzi ya kupigwa mabao 5-1 na Yanga, huku Namungo nayo iliwabana na kutioka nao sare ya 1-1 timu ikiwa kwa kaimu kocha mkuu, Dani Cadena.
Mapema wakati akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Benchikha aliweka wazi anamalizana na mechi za CAF ili kuhakikisha wanavuna pointi za kutosha kuwavusha kwenda robo fainali na ikiwezekana kuvuka hadi fainali na kubeba taji la Afrika na iwapo mambo yatayumba atakomalia kubeba taji la Ligi Kuu.
Kwa sasa taji hilo linashikiliwa na Yanga kwa msimu wa pili mfululizo na Benchikha atakuwa na kibarua cha kulirejesha kwa kufanya kweli kwenye mechi za timu hiyo katika Ligi Kuu.
“Sitaangalia nani anaongoza Ligi au tupo kwenye nafasi ipi, muhimu kwangu na timu kwa jumla ni kubeba taji la Ligi Kuu na michuano mingine tunayoshiriki, mie sio mtu wa mambo nusunusu,” alikaririwa Benchikha alipozungumza na Mwanaspoti.
Tangu atue Msimbazi, Benchikha ameisimamia timu hiyo kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa, ikiwamo ile ya Jwaneng Galaxy uliopigwa jijini Francistown, Botswana na kumalizika kwa suluhu na jana alikuwa tena ugenini kuivaa Wydad.