Kocha Mkuu wa Klabu ya Singida Black Stars (zamani Ihefu FC) amesema kuwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha alimrahisishia kazi baada ya kumtoa nyota wake, Clatous Chama.
Mexime amesema hayo jana baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba huku akifanikiwa kuwabana mbavu Wekundu hao wa Msimbazi na kutoa sare ya bao 1-1 katika Dimba la CCM Liti Singida.
"Mwalimu wao (Benchikha) aliturahisishia pale mwishoni alipomtoa Chama, alikuwa ndio mbunifu. Umeona hata goli tulilofungwa la penati alipigiwa yeye akaingia nao mpira kwenye shimo halafu akautoa mpira kwa Kibu, Kibu akaingia nao ndani akapigwa wakapata penati.
"Kwa hiyo alivyotoka na sisi kidogo ikawa tumebadilisha mpango wetu maana tumepata ahueni na yule tuliyempa kazi ya kumkaba Chama nikambadilishia kazi nyingine.
"Benchikha alishawahi kunifunga (3) nikiwa na Kagera kwa hiyo najua uimara wake uko wapi, nilifanya homework nikajua maeneo gani tukiziba na maeneo gani tukiwaachia wacheze tunaweza kufanikiwa, tumekwenda tumefanikiwa tumepata alama moja sio mbaya.
"Alama moja kwa timu kubwa hizi za Yanga na Simba ni mafanikio japo tulistahili kushinda kwa kuwa tulicheza vizuri. Ukivaa kofia yangu ndio utajua ugumu wa kuwazuia hawa Yanga na Simba, Simba wamecheza vizuri niwapongeze," amesems Mecky Mexime.