Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha aanika 'siri' itayowabeba

Benchikha Juliet Pc Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha.

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zikiwa zimebakia saa chache kabla ya kuwavaa wenyeji Asec Mimosa, Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, amewaambia wachezaji wake mbinu pekee ya kushinda mechi ya kesho ni kuzidisha umakini wanapokuwa na mpira, kutokuwa na presha.

Simba itashuka kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, jijini Abidjan, Ivory Coast kuanzia saa 4:00 usiku kuwakabili wenyeji katika mechi ya raundi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikihitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali.

Benchikha amewaambia wachezaji wake ili kuhakikisha wanavuna matokeo chanya, wanatakiwa kuepuka kufanya makosa ya binafsi na ya kitimu.

Kocha huyo amesema kiufundi ni ngumu kucheza na timu ambayo haina presha na imeshatimiza malengo yake kwa sababu  hawaogopi kufanya makosa uwanjani, badala yake wachezaji wa Simba ndiyo wanatakiwa kuongeza umakini.

"Ni mechi ngumu kiufundi kwa sababu tunacheza na timu ambayo haina presha, imetulia na haina wasiwasi na matokeo yoyote yatakayotokea, imeshatimiza malengo yake ya kutinga hatua ya robo fainali, kucheza na timu ya aina hii ni tabu sana," amesema Benchikha, raia wa Algeria.

Ameongeza amewataka wachezaji wake wawe watulivu na kuhakikisha hawapotezi mipira kirahisi ili kujiweka katika mazingira ya kutawala mchezo lakini pia kujitahidi kupunguza makosa.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano na klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema tangu walipofika Ivory Coast hakuna figisu yoyote waliyokutana nayo, na ametamba Asec Mimosas haina ubavu wa kuifanyia Simba vitu vya 'hujuma' ingawa wamechukua tahadhari zote.

Amesema mchezo wa kesho utakuwa ni wa nyota tano kwa sababu Asec Mimosas ni timu bora, lakini kwao watashuka 'kufa na kupona' kusaka matokeo ya ushindi peke.

Mratibu wa Simba, Abbas Ally, mbali na kusema hali ya hewa ya jiji hilo haina tofauti ya ya Dar es Salaam, inaonekana mashabiki wa soka nchini humo ni kama wamestukizwa kwa sababu bado  walikuwa na furaha ya timu ya taifa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

"Hapa wanachozungumzia ni mafanikio wa timu yao kutwaa Kombe la AFCON, na mechi hii ni kama imewashtukiza, walikuwa wamesahau hivi, furaha ilikuwa imewazidi na hawakujua kama mechi ya Ligi ya Mabingwa itapigwa mapema hivi japo ratiba ilishapangwa kitambo," amesema mratibu huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live