Wakati kikosi cha Simba SC kikirejea kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Mzunguko watatu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, Kocha Mkuu wa kikosi hicho Abdelhak Benchikha ameahidi kuibadilisha timu yake icheze kama anavyotaka yeye.
Simba SC inaelekea katika mchezo huo wa ugenini, ikihitaji matokeo mazuri ili kujisafishia njia ya kuwa moja ya timu mbili zitakazotinga Robo Fainali, kupitia Kundi B.
Kocha huyo aliyejiunga hivi karibuni akitokea USM Alger ya Algeria, amesema kwa jinsi alivyokiona kikosi chake bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na kitabadilika.
“Tunalazimika sasa kushinda kwenye mechi zetu zinazofuata, na kufunga mabao mengi pia, nilichofurahi kwenye mechi iliyopita ni mabadiliko kidogo kwa wachezaji wangu, lakini kuna tatizo kwenye uamuzi, na kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na kuyabadilisha ili kuendana na muundo wa soka la kisasa, hili nitaanza kulifanyia kazi mazoezini,” amesema kocha huyo ambaye mpaka Simba SC inacheza mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi Jwaneng Galaxy nchini Botswana Jumamosi iliyopita hakuwa ameifundisha timu hiyo zaidi ya siku tatu.
Benchikha amesema anataka kutengeneza timu itakayocheza mifumo tofauti, kujiamini, kasi inapoingia kwenye eneo la hatari pamoja na kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi,” amesema.
Hata hivyo, baadhi ya Wanachama na Mashabiki wa Simba SC pamoja na kwamba timu yao ilitoka suluhu, lakini wameonekana kuridhishwa na uchezaji wa timu yao, huku wakienda mbali zaidi kwamba tangu msimu huu uanze katika mechi zote za kimafaifa na Ligi Kuu, wachezaji wa timu hiyo kwa mara ya kwanza wamecheza kwa kiwango cha kuridhisha, hivyo wengi kuwa na imani na kocha huyo kama akikaa na kuifundisha kwa muda mrefu kidogo.
Simba SC wanatarajia kushuka dimbani Desemba 9, mwaka huu, wakiwa ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Grand stade de Marrakech, uliopo Marrakech, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.