Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha: Nataka straika huyu haraka sana

Benchikha Morocco.jpeg Benchikha: Nataka straika huyu haraka sana

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Dakika 90 za mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi Simba ikiwang'oa kwa matuta Singida Fountain Gate zimempa kocha Abdelhak Benchikha akili mpya.

Benchikha amewaambia viongozi wa klabu hiyo kwamba suala la usajili wa mshambuliaji mwenye shabaha ya kutupia, haliepukiki na linatakiwa kufanyiwa uamuzi wa haraka.

Amewaambia kuwa bado Simba inahitaji mshambuliaji mwenye msuli wa kuwapangua mabeki na kufunga ili kikosi chake kipate nguvu kubwa haswa kwenye mashindano yaliyoko mbele yao.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliyeko kwenye jopo la usajili ameiambia Mwanaspoti kuwa kocha amekuwa mkali kupita wakati mwingine wowote.

Ametaka kujua mchakato wa usajili wa mastaa wawili anaowataka haswa pale kwenye safu ya mbele umefikia wapi huku akisisitiza mshambuliaji wa kati anatakiwa kutangulia fasta kwani waendako ni kugumu na hawawezi kutoboa kwa picha aliyoiona mpaka sasa kwenye Kombe la Mapinduzi.

Benchikha amewaambia haridhishwi na viwango vya washambuliaji wake Jean Baleke na Mosses Phiri ambao waligawana dakika 45 za mechi ya nusu fainali dhidi ya Singida lakini hawakufunga bao lolote ndani ya muda waliokuwa uwanjani.

Baleke amefunga mabao mawili ndani ya mechi tano alizocheza kwenye mashindano hayo huku Phiri aliyekuwa akitetewa zaidi na mashabiki wakitaka aanze kwenye kikosi cha kwanza akifunga bao moja.

"Kocha anataka matokeo mazuri zaidi anaona bado nguvu yetu kule mbele haimfurahishi tunapambana kutafuta mtu wa maana wa pale mbele ili hawa tulionao wawe watu wa kuja kuongeza kitu baadaye na sio kuwategemea kama chaguo la kwanza," alidokeza kiongozi huyo wa Simba ingawa hakuweka wazi kwamba watanunua mchezaji kutoka nchi gani.

Benchikha akizungumzia mechi hiyo ya jana amesema kikosi chake kimecheza mechi moja ngumu ya ndani dhidi ya timu Bora ambayo imempa nafasi ya kujua maboresho zaidi ambapo Sasa anakwenda kutafanyia kazi.

"Hii ni mechi Moja ngumu dhidi ya timu Bora, ukipata kipimo Cha namna hii kinakupa nafasi ya kujua kazi mnayofanya ina ubora wa namna gani au wapi mnatakiwa kuongeza kitu," amesema Benchikha ambaye kwa sasa ana miaka 60 na ana uzoefu mkubwa kwenye soka la Afrika.

"Kuna maeneo tunahitaji kuongeza nguvu au Kuna wachezaji wanatakiwa kuongeza kasi ya kutupa ambacho timu inahitaji, changamoto yetu kubwa ipo hapa tutaendelea kufanya kazi ya kuboresha mambo ambayo tumeyabaini," alisema Benchikha ambaye timu yake inacheza dhidi ya Asec Februari 23 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imebakiza siku tano kuanzia leo kuhakikisha malengo yao hayo yanatimia kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili Januari 15. Endelea kufuatilia kila kinachojiri kwenye usajili wa Simba kupitia kwenye mitandao yetu.

Chanzo: Mwanaspoti