Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha: Kuna mengi ya kuibadilisha Simba

BENCHIKHA New.jpeg Benchikha aahidi mabadiliko makubwa Simba

Thu, 7 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Simba tayari kimerejea kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, Kocha Mkuu wa kikosi hicho Abdelhak Benchikha ameahidi kuibadilisha timu yake icheze kama anavyotaka yeye.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha huyo aliyejiunga hivi karibuni akitokea USM Alger ya Algeria, amesema kwa jinsi alivyokiona kikosi chake bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na kitabadilika.

“Tunalazimika sasa kushinda kwenye mechi zetu zinazofuata, na kufunga mabao mengi pia, nilichofurahi kwenye mechi iliyopita ni mabadiliko kidogo kwa wachezaji wangu, lakini kuna tatizo kwenye uamuzi.

"Na kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na kuyabadilisha ili kuendana na muundo wa soka la kisasa, hili nitaanza kulifanyia kazi mazoezini,” alisema kocha huyo ambaye mpaka Simba inacheza mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi Jwaneng Galaxy nchini Botswana Jumamosi iliyopita hakuwa ameifundisha timu hiyo zaidi ya siku tatu.

 Kocha huyo alisema anataka kutengeneza timu itakayocheza mifumo tofauti, kujiamini, kasi inapoingia kwenye eneo la hatari pamoja na kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba pamoja na kwamba timu yao ilitoka suluhu, lakini wameonekana kuridhishwa na uchezaji wa timu yao, huku wakienda mbali zaidi kwamba tangu msimu huu uanze katika mechi zote za kimafaifa na Ligi Kuu, wachezaji wa timu hiyo kwa mara ya kwanza wamecheza kwa kiwango cha kuridhisha, hivyo wengi kuwa na imani na kocha huyo kama akikaa na kuifundisha kwa muda mrefu kidogo.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi kilitarajia kuanza mazoezi jana saa tisa kwenye Uwanja wa Mo Arena, Bunju, Dar es Salaam na moja kwa moja kuingia kambini kwa ajili ya mechi dhidi ya Wydad Casablanca inayotarajiwa kucheza Jumamosi kwenye Uwanja wa Marrakech nchini Morocco.

“Tuliporejea tuliwapa mapumziko kidogo wachezaji wetu, lakini wanarejea leo (jana), saa tisa na kuanza rasmi mazoezi na kambi kwa ajili ya mechi ya tatu dhidi ya Wydad, ni mechi ngumu kwa sababu jamaa wamepoteza zote mbili za mwanzo, hivyo watataka kuamkia kwetu, lakini na sisi tunajipanga, kwa siku hizi kadhaa nadhani kocha wetu atapandikiza ujuzi na ufundi wake kwa wachezaji.

“Tumeona siku chache tu baada ya kuichukua timu kuna kitu kimeanza kuonekana, nadhani baada ya muda kidogo timu itakuwa sawa, umeona wachezaji wanajituma, wanakimbia, na hata utimamu wa mwili umeanza kuongezeka,” alisema Ahmed.

Asec Mimosas inaongoza Kundi B, ikiwa na pointi nne na mabao mawili, sawa na Jwaneng Galaxy inayoshika nafasi ya pili, lakini yenyewe ina bao moja, Simba ikiwa namba tatu kwa pointi mbili na Wydad ikiburuza mkia bila pointi.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Baleke amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo na kusema bado wananafasi ya kusonga mbele  kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapoenda  kusaka alama tatu dhidi ya Wydad Casablanca.

Amesema hadi sasa wana pointi mbili na wanaimani kubwa ya kupata pointi tatu za mchezo dhidi ya wenyeji wao, Wydad Casablanca ugenini ili waweze kufikisha pointi tatu muhimu kwa ajili ya kufikia malengo yao.

Akizungumza na Nipashe, Baleke aliwaomba msamaha mashabiki wa Simba kwa matokeo ya nyuma na kuwataka kuungana kuwa nguvu mmoja kuelekea kwenye mechi hiyo dhidi ya Wydad. Alisema wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo, na kwamba wanahitaji kufanya vizuri kwa sababu malengo yao ni kuona Simba inasonga mbele kuvuka makundi na kucheza robo fainali.

“Samahani mashabiki wetu, tusahau matokeo yaliyopita ambayo kocha wetu (Abdelhak Benchikha) amefanyia kazi mapungufu yetu sasa nguvu na akili zetu tumezielekeza kusaka ushindi dhidi ya Wydad Casablanca,” alisema Baleke.

Kuhusu tetesi za kutakiwa kurejea katika klabu yake ya TP Mazembe, Baleke alisema bado yupo na ni mtoto wa Simba, anachokifikiria zaidi ni kuona timu yake inafanikiwa kuvuka katika hatua ya makundi na kwenda robo hatimaye nusu fainali.

Simba wanatarajia kushuka dimbani Desemba 9, mwaka huu, wakiwa ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Grand stade de Marrakech, uliopo Marrakech, saa 4:00 usiku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live