Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha, Gamondi wamepata majibu Kombe la Mapinduzi 2024

Benchikha X Gamondi Benchikha, Gamondi wamepata majibu Kombe la Mapinduzi 2024

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna shaka michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 imekuwa kipoozeo chema kwa mashabiki wa soka ambao wanalazimika kusubiri hadi Februari 14 kuanza tena kuona timu zao pendwa zikiendelea kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.

Kipindi hiki, ligi zimelazimika usimama kwa muda kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) ambazo zinafanyika Januari hii, 2024, kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri katikati ya mwaka, muda ambao fainali hizo huwa zinachezwa.

Ni utamaduni wa nchi zote duniani, timu ya taifa inapopambana, mashindano mengine yote yanasimama ili kuwapa mashabiki fursa ya kuishuhudia timu yao ikipeperusha bendera ya taifa.

Ni kwa mantiki hiyo, Ligi Kuu inalazimika kusimama. Ni tofauti na huko nyuma, timu yenye idadi fulani ya wachezaji kwenye timu ya taifa, ndiyo pekee iliyoahirishiwa mechi zake za Ligi.

Hata hivyo, kwa sasa hata timu isipokuwa na mchezaji kwenye timu ya taifa, inanufaika na mapumziko hayo.

Kipindi hiki cha mwanzoni mwa Januari ndicho hutumiwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuendesha mashindano yanayozidi kuwa maarufu ya Kombe la Mapinduzi, kuenzi Mapinduzi ya visiwa hivyo yaliyouondoa utawala wa kisultani Januari 12, 1964.

Kwa kawaida, kipindi hiki pia huwa ni cha mapumziko, hivyo klabu huruhusu wachezaji kupumzika isipokuwa kwa sababu maalum.

Hata hivyo, timu ambazo hupata mwaliko wa kushiriki Kombe la Mapinduzi huwa haziruhusu wachezaji wake kwenda kupumzika na badala yake hutumia mashindano hayo kuimarisha vikosi vyao na hata kujiongezea rekodi kwa kutwaa ubingwa au angalau kufika fainali.

Lakini si kwa Simba na Yanga. Mara nyingi, vigogo hao wa Kariakoo huruhusu wachezaji wa vikosi vya kwanza kwenda mapumziko, huku wale ambao hawakupata muda wa kutosha, wakienda na timu Zanzibar ili kuangaliwa zaidi na makocha, hasa wasaidizi.

Hali imekuwa tofauti mwaka huu. Miguel Gamondi wa Yanga na Abdelhak Benchikha, kwa sababu tofauti wameambatana na timu visiwani Zanzibar kwenda kuweka mambo sawa wakati huu wa mapumziko mafupi ya msimu.

Ilikuwa ni dhahiri kwa Benchikha kutoruhusu wachezaji ambao hawajaitwa na nchi zao kuambatana nao Zanzibar. Hii ni kwa sababu kocha huyo Mualgeria ndio kwanza amekabidhiwa timu baada ya mtangulizi wake, Roberto Oliveira “Roberinho’ kutimuliwa.

Ameichukua timu wakati ikiwa ndio kwanza imeanza msimu na ikiwa na matokeo yasiyoridhisha kulinganisha na mpinzani wake, Yanga, huku ikiwa na kibarua kigumu kwenye Ligi ya Mabingwa wa Afrika ambako inapambana na vigogo kama Wydad Athletic na Asec Mimosas kujaribu kufikia tena hatua ya robo fainali na hasa nusu fainali ambayo imekuwa mtihani mkubwa kwa vijana hao wa Mtaa wa Msimbazi.

Kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kwa Benchikha kujaribu wachezaji zaidi ya wale ambao walikuwa wakitumiwa na mtangulizi wake, ingawa amejaribu katika baadhi ya maeneo kama golini ambako ameshajaribisha makipa watatu hadi sasa, na kidogo kwenye safu ya ushambuliaji ambako amemwamini Willy Onana na kumpa muda kidogo kiungo kipenzi cha mashabiki, Clatous Chama.

Hangeweza kufanya uthubutu mkubwa katikati ya mashindano, lakini imekuwa bahati amekutana na Kombe la Mapinduzi ambalo limempa fursa ya kujaribu wachezaji wengi, hadi wale wa timu ya vijana na ambao wanategemea kusajiliwa.

Bila shaka hadi kumalizika kwa mashindano hatakuwa na maswali kichwani kuhusu nani amuanzishe mechi ya aina fulani na nani aanzie benchi. Na sidhani kama kutakuwa na maswali zaidi ya sababu za kutomchezesha mchezaji fulani na kuanza na mchezaji fulani.

Benchikha aliweka bayana kuwa ataitumia michuano hii kuimarisha kikosi chake na hivyo matarajio ni atakuwa na majibu yote wakati awamu ya pili ya Ligi Kuu itakapoanza tena.

Hali ni tofauti kwa Gamondi. Ameenda mapumziko akiwa na moja ya vikosi bora msimu huu, akiwa amepoteza mchezo mmoja dhidi ya Ihefu, mchezo ambao ulitoa majibu machache kuhusu kuzungusha wachezaji kwa lengo la kupumzisha baadhi na kuwapa wapinzani ladha tofauti inaowafanya wasijiandae vizuri kuwakabili vijana hao wa Jangwani.

Alienda mechi ya Ihefu akilaumiwa anatumia wachezaji walewale tofauti na mtangulizi wake, Nasredine Nabi, ambaye ameondoka akiwa ametumia takriban asilimia 70 ya wachezaji waliosajiliwa kutokana na mfumo wake wa kujaribisha kila mchezaji (rotation) uliompa sifa.

Katika mechi hiyo, Gamondi alipumzisha zaidi ya asilimia 50 ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na akakumbana na kipigo cha mabao 2-1, ikiwa ni kama marudio ya mechi ya msimu uliopita wakati timu hiyo ya mkoani Mbeya ilipositisha wimbi la ushindi wa mechi 49 kwa Yanga.

Gamondi alipumzisha baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza wakati timu ikienda Zanzibar na baadhi walikuwa wameitwa nan chi zao kujiandaa kwa Afcon 2023. Naye aliweka bayana kuwa ataitumia michuano hiyo kutoa nafasi kwa wachezaji ambao walikuwa hawapati muda wa kutosha au ambao hajawatumia kabisa.

Baada ya mechi mbili za kwanza, Muargentina huyo alielezea lawama alizokuwa akipata kutoka kwa mashabiki kuwa anategemea zaidi wachezaji wa kikosi cha kwanza wakati ana jeshi kubwa la wachezaji nyota. Gamondi amesema ametumia Kombe la Mapinduzi kutoa nafasi kwa wachezaji wengi, lakini anaona tofauti kubwa akilinganisha na wachezaji anaowatumia.

Kocha huyo kutoka Amerika Kusini amesema wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wana kiwango cha juu kulinganisha na hawa anaowajaribu na wengi hawajitumi sana, akitaka kuwaonyesha wanaomkosoa kuwa hana jeshi kubwa kama inavyofikiriwa.

Ni dhahiri si wote hawafikii viwango anavyotaka na wala hajaona kitu zaidi kwa wachezaji ambao alikuwa hawatumii, lakini anaondoka na majibu ambayo alitamani wengi wayashuhudie hadharani ili atakapoendelea na mipango yake msimu utakapoendelea asiulizwe maswali mengi.

Kwa kawaida kile wanachosema mashabiki huwa hakitofautiani sana na kile baadhi ya viongozi wanachofikiria na hivyo majibu yaliyopatikana Kombe la Mapinduzi yatakuwa yamempa ahueni Gamondi wakati atakapokuwa akipanga timu kwa ajili ya kumalizia kazi ya kutetea kombe ambalo mtangulizi wake alilitwaa kwa misimu miwili mfululizo.

Hakuna shaka maswali ambayo Benchikha na Gamondi walikuwa wakikabiliana nayo kila mechi zinapoisha, yatakuwa yamepata majibu, labda tu kuhusu wale nyota wanaosajiliwa au kutambulishwa usiku wa maanani ambao baadhi wanaweza wasijaribiwe Kombe la Mapinduzi.

Zaidi ya hapo, maswali yote yamepata majibu na kama yapo yatakayoibuka baada ya hapo, yatakuwa ni ZENGWE.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live