Klabu ya Azam FC rasmi imejiengua kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuchemsha kwenye baadhi ya michezo iliyocheza hadi sasa na kusaliwa na vita ya michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ Benchi la Ufundi la timu hiyo limeamua kujitathmini ili kujiweka sawa.
Kocha msaidizi wa Azam, Kally Ongala amesema kwa hatua ambayo timu hiyo imefikia imebidi Benchi la Ufundi pamoja na wachezaji wajitathmini ili kufanya vizuri katika michezo iliyosalia msimu huu 2022/23.
Azam FC inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 47 baada ya kucheza michezo 25 huku mwanzoni mwa msimu ilianza vizuri na kuonyesha inaleta ushindani katika Ligi hiyo.
Ongala amesema kitendo cha kutokuwa na matokeo mazuri kiliwavuruga wachezaji kisaikolojia lakini wamekaa nao chini na kuwaweka sawa na ana imani watakuwa na matokeo mazuri katika michezo iliyosalia.
“Tumejitafakari, tumeongea na wachezaji wetu na kikubwa tumewaambia wanatakiwa kupambana kwa kila ambaye anapata nafasi ya kucheza,” amesema Ongala na kuongeza;
“Wachezaji wanatakiwa kujitafakari lakini na sisi Benchi la Ufundi tufanye hivyo lengo likiwa ni kurudi katika hali yetu ya kawaida katika mechi zilizosalia.”
Ongala amesema ni lazima kubadilisha mwenendo mbaya na kupambana hadi mwisho na itakuwa nzuri kwa mchezaji mwenyewe na hata timu pia.
“Tumeongea na wachezaji kwa hiyo imani yetu tutakuwa vizuri, maneno yetu sasa yanaenda kwenye vitendo kupata matokeo mazuri kwenye michezo yetu,” amesema Ongala