Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchi jipya, matumaini mapya Stars

Hanour Janza Janza Mzambia Honour Janza ambaye anakinoa pia kikosi cha Namungo akisaidiwa na mzawa Mecky Mexime

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uganda katika mechi ya kuwania nafasi ya kufuzu michuano ya kimataifa kwa wachezaji wa ndani Afrika (Chan), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifikia makubaliano ya kumuondoa kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Kim Poulsen kwenye benchi la ufundi pamoja na wasaidizi wake.

Stars ambayo inatarajiwa kukutana na Uganda Septemba 3, mwaka huu kukamilisha mchezo wa marudiano nchini Uganda, kwa sasa itakuwa chini ya Mzambia Honour Janza ambaye anakinoa pia kikosi cha Namungo akisaidiwa na mzawa Mecky Mexime na kocha wa makipa Juma Kaseja.

Uamuzi wa kuondolewa kwa Poulsen ni makubaliano ya pande zote mbili kati yake na TFF baada ya kikao cha pamoja na licha ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi, lakini ataendela kubaki katika timu za taifa kwa vijana hadi pale mkataba wake utakapokwisha.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi mfupi juu ya benchi jipya la Stars linalokabiliwa na kibarua cha kuiongoza Stars kufuzu Chan mwakani nchini Algeria.

HONOUR JANZA

Janza ana uwezo kwenye kufundisha timu ya taifa kwani aliwahi kufanya hivyo baada ya kuteuliwa kuifundisha timu ya taifa Zambia ‘Chipolopolo’ Agosti 6, 2014.

Kocha huyo alichukua nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Mfaransa Patrice Beaumelle ikiwa ni miezi tisa tu aliyodumu kufuatia kuondoka kwa Herve Renard aliyetimkia Ivory Coast.

Janza alikiongoza kikosi hicho kwenye michuano ya Mataifa Afrika (Afcon) akawalaumu wachezaji wake kufuatia kufungwa mabao 2-1 na Tunisia na ilipofika Machi 2015 Chama cha Soka Zambia (FAZ) kilitangaza kutafuta mbadala wake na ndipo alipoona kasalitiwa.

Hata hivyo malalamiko hayo kwa Janza hayakubadili uamuzi wa chama hicho kwani ilipofika Juni 2015 aliondolewa na nafasi yake kupewa George Lwandamina.

Kocha huyo katika nyakati tofauti alikuwa akifundisha timu za vijana za Zambia na pia amekuwa akiteuliwa kuwa kocha msaidizi timu ya taifa.

JUMA KASEJA

Kipa huyu mkongwe nchini msimu uliopita alikuwa akiitumikia KMC, lakini baada ya kuachwa aliweka bayana yupo tayari kuichezea timu yoyote hata Championship.

Wakati akisikilizia dili jipya TFF imeona anafaa kuchukua nafasi ya kuwanoa makipa wa Stars kutokana na uzoefu wake kwenye soka la Tanzania.

Kaseja maarufu kama Tanzania One ni mmoja wa wachezaji wazoefu na wamecheza Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu. Amewahi kupita katika timu mbalimbali kama Moro United, Simba, Yanga, Mbeya City na Kagera Sugar akijizoelea umaarufu kutokana na uwezo wake anapokuwa langoni.

Moja ya historia kubwa kwa Kaseja aliyoiweka nchini ni wakati akiichezea Simba 2003 baada ya kuhusika kuwavua ubingwa miamba wa soka Misri, Zamalek kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambayo sasa inatambulika kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nyota wengine walioanza na kaseja kwenye kikosi hicho ni Emmanuel Gabriel, Said Swedi, Yusuf Macho, Christopher Alex, Victor Costa, Seleman Matola, Ramadhani Wasso, Ulimboka Mwakingwe, Athumani Machupa na beki kitasa Boniface Pawasa.

Licha ya kwamba Kaseja anacheza, lakini amepata mafunzo mbalimbali ya ukocha hususan wa makipa katika kozi zinazotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

MECKY MAXIME

Maxime ni kocha mzawa mwenye historia nzuri kwenye soka la Tanzania ambaye amewahi kuwa sehemu ya kikosi cha Mtibwa Sugar kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara zaidi ya mara mbili nje ya Simba, Yanga kikifanya hivyo msimu wa 1999 na 2000 chini ya makocha John Simkoko na msaidizi wake, Ahmed Mumba.

Hadi anajiunga na Taifa Stars, Maxime alikuwa kocha mkuu wa kituo cha kukuza vipaji cha soka cha Cambiasso Sports Management baada ya kuachana na Kagera Sugar aliyowahi kuifundisha akitokea Kagera Sugar.

Mtaalamu huyo wa ufundi wa soka amewahi kuwa nahodha wa Mtibwa Sugar lakini pia Stars katika vipindi tofauti chini ya kocha Mbrazili Marcio Maximo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz