Mchezaji wa Chelsea Ben Chilwell anaamini kuwa wachezaji wenzake wa Chelsea lazima wawajibike kikamilifu kwa mwenendo mbaya wa matokeo katika Premier League na anasema njia pekee ya kubadilisha kiwango cha timu hiyo ni kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Chelsea walipata kichapo cha nane msimu dhidi ya Southampton siku ya Jumamosi, mchezo ambao uliamuliwa na nahodha wao James Ward-Prowse baada ya kupiga mpira wa ‘Free Kick’ na kuingia langoni moja kwa moja.
Kikosi cha Graham Potter kilipiga mashuti 17 kwenye mchezo huo, ikiwa ni idadi kubwa ya mara ya pili kwa timu hiyo kupiga mashuti mengi kwenye ligi kuu msimu mzima, ingawa hawakuweza kupata bao licha ya nafasi nyingi.
Beki wa kushoto wa Chelsea Ben Chilwell, hakutaka kutumia nafasi alizopoteza kama sababu ya kushindwa alipozungumza na vyombo vya habari baada ya mechi.
“Tena, haitoshi. Ninaweza kusimama hapa na kusema tulitengeneza nafasi, kama nilivyosema huko Dortmund, lakini haimaanishi chochote. Tunahitaji kushinda michezo hii,” Ben Chilwell.
“Tunahitaji kufanya kazi kwa bidii, ni chumba kizuri cha kubadilishia nguo kwa sasa. Ni vigumu kuingia ndani yake, kulingana na kile tulifanya haki na makosa leo (Jumamosi), lakini tuna muda sasa hadi mchezo wetu ujao kufanya kazi kwa bidii.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza anaamini kuwa wachezaji wanatakiwa kujipanga upya na kujitazama kabla ya mechi ya London derby dhidi ya Tottenham Hotspur Jumapili ijayo.
“Ni rahisi kusema, lakini lazima tufanye bidii na kubadilisha hili, na watu pekee wanaoweza kufanya hivyo ni sisi wenyewe.
“Si jambo zuri kwa kundi lenye ushindani ambalo linataka kushinda vitu. Baadhi yetu miaka michache iliyopita tulionja kushinda kombe kuu na kisha kuwa katika hali hii sasa, hatujisikii vizuri hata kidogo.
“Inaeleweka kuwa mashabiki hawana furaha. Wanatarajia Chelsea kushinda mechi ambazo pia tunazitarajia.”