Borussia Dortmund imeripotiwa kufuta kabisa mpango wa kushusha bei ya kiungo wao Jude Bellingham, itabaki kuwa ileile hata kama watashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kiungo huyo kinda mwenye umri wa miaka 19 amekuwa gumzo kwenye mazungumzo yanayohusu usajili huko Ulaya, huku klabu kubwa mbalimbali zikipambana kunasa saini yake.
Lakini, Dortmund bado ina mkataba na Bellingham hadi majira ya kiangazi mwaka 2025, lakini kuna uwezekano mkubwa wakaachana naye kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi mwishoni mwa msimu huu.
Liverpool na Real Madrid zimeripotiwa kuchuana vikali kwenye kuwania saini ya Mwingereza huyo, huku miamba ya Anfield ikiwa na uhakika mkubwa Bellingham atakwenda kukipiga kwenye kikosi chao msimu ujao.
Lakini, Real Madrid wao wanataka kumfanya Bellingham abaki Dortmund hadi mwakani kabla ya kumchukua kuja kuvaa buti za viungo maveterani waliopo Bernabeu, Toni Kroos na Luka Modric.
Hata hivyo, Manchester United na Manchester City nazo zinafuatilia kwa karibu mchakato wa kumsajili kiungo huyo wa Dortmund, ambaye timu yake inasema haitakaa mezani kuzungumza biashara kama hakutakuwa na ofa inayoanzia Euro 150 milioni.
Dortmund wamekuwa wagumu kwenye kufanya biashara ya kuwapiga bei mastaa wake na inapofanya hivyo, basi ni kwa mkwanja mrefu kama ilivyomuuza Ousmane Dembele kwenye Barcelona na Jadon Sancho kwenda Man United.