Habari zilizotufikia hivi punde ni kwamba beki wa zamani Tukuyu Stars, Simba na Yanga, Seleman Mathew amefariki dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam.
Beki huyo wa zamani alikuwa katika kikosi cha Tukuyu Stars 'Wana Banyambala' kilichotwaa ubingwa wa Ligi ya Tanzania Bara mwaka 1986 kabla ya kupita katika klabu mbalimbali ikiwamo Ndovu Arusha, Simba na Yanga.
Katika kikosi cha Tukuyu kilichobeba ubingwa wa Bara 1986 Mathew alikuwa pamoja na Kevin Haule, Hussein Zitto, Karabi Mrisho, Godwin Aswile, Ally Kimwaga, Danford Ngessi, Mbwana Makata, Fadhil Hembe, Richard Lumumba, Yusuph Kamba, John Alex, Daniel Chundu, Aston Pardon na nahodha akiwa Peter Mwakibibi, huku kocha akiwa Athuman Juma chini ya ulezi wa Ramnick Patel ‘Kaka’.
Mathew alipoachana na soka aliingia katika siasa akiwania na kushinda udiwani Kata ya Vijibweni mwaka 2012 kupitia Uchaguzi Mdogo akiwa CCM kabla ya kuhamia Chadema na kuwahi kupambana na Nape Nnauye katika Ubunge Jimbo la Mtama Uchaguzi Mkuu wa 2015.