Khatimu Naheka, Mwananchi
Dar es Salaam. Beki wa Yanga Gadiel Michael ameondoka nchini kwenda kufanya majaribio ya wiki mbili imefahamika.
Gadiel ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Stars amepata mualiko huo ikiwa ni siku chache baada ya kuisaidia Stars kufuzu Fainali za Mataifa Afrika mwaka huu 2019.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ambazo Mwanaspoti limethibitishiwa ni kwamba mualiko huo ulikuwa wa muda mrefu lakini kiwango alichokionyesha beki huyo katika mchezo dhidi ya Uganda kimechangia.
Tayari klabu yake ilishatoa baraka zote kwa Gadiel akitua katika klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini inayoshiriki ligi kuu nchini humo.
Endapo Gadiel atafuzu majaribio hayo huenda ikawa fursa nyingine kwa Yanga kuongoza fedha endapo biashara itafanyika baina ya timu hizo mbili kutokana na bado beki huyo yupo ndani ya mkataba na Yanga.
Kufuatia taarifa hizo Mwanaspoti lilimtafuta Mratibu wa Yanga Hafidh Saleh ambaye alithibitisha beki huyo kuwepo nchini Afrika Kusini.
“Nikweli Gadiel hayupo nchini na uongozi unataarifa amekwenda Afrika Kusini kwenye majaribio ya wiki mbili tunamtakia kila la kheri katika safari yake hiyo,” alithibitisha Saleh.