Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Beki kisiki wa Nigeria ageukia uchungaji

Taribo West Kisiki Beki wa zamani wa Nigeria, Taribo West

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Aliyekuwa beki kisiki, kiboko ya Thierry Henry huko kwenye Ligi Kuu England, ameamua kuwa mchungaji nyumbani kwao Nigeria.

Taribo West, beki mwenye roho ngumu kwelikweli, ambaye alikuwa maarufu pia ndani ya uwanja kutokana na staili ya kipekee ya nywele.

Beki huyo alikuwa moto mwishoni mwa miaka ya 1990, akishinda taji la Ligue 1 alipokuwa kwenye kikosi cha Auxerre mwaka 1996.

Baadaye alienda kuzichezea AC Milan na Inter Milan kabla ya kuhamia kwenye Ligi Kuu England kukipiga kwenye kikosi cha Derby mwaka 2000.

Si mabeki wengi walijua namna ya kumdhibiti straika wa Arsenal, Thierry Henry, lakini West alikuwa mchezaji ambaye staa huyo wa Ufaransa hakupenda kabisa kukutana naye uwanjani.

Henry alisema West alikuwa mmoja kati ya mabeki wagumu zaidi aliowahi kukabiliana nayo, akisema: “Wale Auxerre walikuwa wakikaba mtu na mtu. Anakufuata kila mahali, hadi kwenye vyumba vya kubadilishia.”

Lakini, sasa West ameamua kumfuata Mungu na si washambuliaji hatari.

West, 49, alisema amekuwa na bahati kubwa kwa muda wote aliokuwa mwanasoka. Baada ya kustaafu, badala ya kufanya ukocha, aliamua kuhamia kwenye kumtumikia Mungu na kuwa mchungaji, ambapo alianzisha kanisa mwaka 2014.

Alisema: “Kwanini nimebadili kutoka kuwa mwanasoka hadi kuwa mchungaji? Nimemuona Mungu. Hapo ndipo nilipoanzia,” alisema.

Kabla ya kuwa mtumishi, West anadai soka limekuwa mwokozi wake, la sivyo angekuwa kijana wa hovyo kwelikweli mtaani kutokana na maisha aliyokulia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live