Klabu ya ya Arsenal, imepokea taarifa mbaya ya majeraha ya beki wa timu hiyo, Jurrien Timber kutoka kituo cha habari huko Uholanzi.
Beki huyo alipata jeraha baya la goti mwanzo wa msimu na huenda akakosekana muda wote ambao umebaki wa msimu huu.
Beki huyo aliyeumia vibaya kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Nottingham Forest, alisajiliwa kwa Pauni 38 milioni kipindi cha usajili wa kiangazi akitokea Ajax.
Sasa Arsenal imepata hofu baada ya taarifa kutoka Uholanzi kuthibitisha tarehe ya kurejea kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa taifa hilo.
Na ripoti hiyo inadai kuna uwezekano wa Timber kurejea dimbani mwakani kwenye kikosi cha Uholanzi kitakachoshiriki michuano ya Euro huko Ujerumani.
Kulikuwa na matumaini beki huyo angerejea karibia na msimu kumalizika lakini kufuatia upasuaji aliofanyiwa, kuna uwezekano asionekane kabisa hadi msimu mpya unaokuja.
Beki huyo aliongeza uimara kwenye safu ya ulinzi licha ya kucheza dakika 50 tu tangu alipotua, kwani alimshawishi Arteta baada ya kuisaidia Ajax kutwaa mataji mawili ya Eredivisie na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi msimu wa 2021-22.
Baada ya Mdachi huyo kuumia, Arteta alilazimika kuwarejesha kwenye kikosi Takehiro Tomiyasu na Oleksandr Zinchenko.
Licha ya kumkosa Timber kwa muda mrefu Arsenal imeendelea kufanya vizuri na inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kesho itacheza dhidi ya Brentord baada ya mapumziko ya ligi kupisha mechi za kimataifa kumalizika yaliyodumu kwa muda wa wiki mbili.
Arsenal ina pointi 27 kwenye msimamo, sawa na Liverpool iliyo katika nafasi ya pili, zote zikizidiwa pointi moja na vinara, Man City.