Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Beki Yanga: Chama, Pacome ndo wenyewe sasa!

Pacome Zouzoua Nov.jpeg Beki Yanga: Chama, Pacome ndo wenyewe sasa!

Sun, 18 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Unaikumbuka ile Yanga iliyopigwa 5-0 na Simba katika mechi ya Kariakoo Derby iliyopigwa Mei 6, 2012?

Kama hujui ni kwamba Yanga ile ilikuwa na watu kwelikweli waliojaliwa vipaji, nguvu na akili, lakini sijui kiliwakuta nini hata wakatandikwa mkono kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa?

Katika mechi hiyo kuna watu waliishia kulia wakiwa benchi akiwamo Godfrey Taita. Beki huyo aliyemudu pia kucheza kama winga wa kulia alikuwa ni mmoja wa nyota waliounda kikosi cha Yanga cha msimu huo wa 2011 na alikaa na timu hiyo hadi mwaka 2013 kabla ya kutimka zake Villa Squad.

Yanga ilimnasa mchezaji huyo ambaye kwa sasa amestaafu akitokea Kagera Sugar alikokiwasha sana. Walimuona ni mtu anayeweza kuvaa viatu vya Shadrack Nsajigwa na kusaidiana naye pale Jangwani na jamaa alikula sahani moja na Fuso kabla ya kuhamishiwa eneo la mbele kama winga.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na mkongwe huyo na kufunguka mambo mengi, ikiwamo kufichua namna Yanga ilivyompa mjengo wa maana sambamba na kujitofautisha na wengine na pia kuwaumbua waliokuwa wakimuona kuwa ni mchezaji mhuni flani, huku akiwataja Clatous Chama na Pacome Zouzoua waliopo Simba na Yanga kama miongoni mwa mastaa wanaomkuna kwa viwango bora uwanjani. Tiririka naye kupata uhondo mtamu kupitia mahojiano hayo maalumu yaliyozaa makala haya. Endelea...!

AKILI NYINGI

Wale waliosema akili ni nywele na kila mtu ana zake, hawakukosea, kwani Taita aliyezaliwa  Februari 26, 1986 anafichua tangu aache kucheza soka la ushindani na kuwa kimya, hajakaa kizembe, bali anapambana kutengeneza kesho yake na watoto wake kwa kutambua maisha huwa hayarudi nyuma.

Taifa anasema kuna watu walipambana kumfanya aonekani kama mhuni, lakini ukweli hayupo hivyo anaishi kwa akili na kufanya mambo ya maendeleo kimya kimya, akifichua huwa hapendi kuigiza maisha bali kuishi na kufanya kitu halisi kwa sababu anajiamini maisha yake ni yake na sio ya wengine.

“Kuna wakati mwingine tunapoteza nguvu kuwaaminisha watu uzuri wetu, nadhani mimi sina mchongo huo, badala yake nafikiria zaidi kufanya maendeleo binafsi. Maisha hayarudi nyuma,” anasema Taifa ambaye aliacha soka la ushindani mwaka jana ili kusimamia mirathi ya mama yake, marehemu Rehema Maganga aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Kisutu na Mnazi Mmoja zilizopo jijini Dar es Salaam.

KASHFA STARS

Katika stori za hapa na pale anaulizwa na Mwanaspoti ni tukio gani hatakaa alisahau kwenye maisha yake ya soka, lakini kabla ya kujibu aliinama chini na uso wake kubadilika kutoka kwenye kicheko na kuonekana mtu mwenye mawazo hivi.

Inamchukua kama dakika moja kuamua kulisimulia tukio la kutuhumiwa kuingiza mwanamke kwenye kambi ya timu ya taifa.

“Tukio lenyewe lilikuwa hivi, nilishangaa napigiwa simu na Sunday Kayuni. Nikaipokea na kumwamkia akaniuliza Taita umefanya kitu gani hapo kambini, nikamjibu sijafanya jambo lolote. Akauliza tena hujaingiza mwanamke kambini, nikamjibu siwezi kufanya jambo kama hilo,” anasema mchezaji huyo.

“Baada ya kukata simu nikawaona kocha  Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na nahodha Juma Kaseja wakachungulia chumbani kisha wakaondoka. Baada ya muda kocha Julio aliniambia Taita beba begi lako rudi nyumbani.

“Kabla ya kuondoka kiongozi wa Yanga alipiga simu. Alikuwa Seif Ahmed ‘Magari’ aliniuliza Taita umefanya nini huko. Nikajibu sijafanya kitu akasema sawa, tukigundua umefanya ujinga huo, tutaenda kuangalia CCTV camera, ukibainika utafukuzwa hatutataka uichafue brand (chapa)ya klabu. Kwa kuwa sikufanya nikawa na amani.”

Anasema akampigia simu dereva akaenda kumchukua kambini na kumpeleka nyumbani kwake, ambako akakuta mkewe amenuna, kwani tayari vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti taarifa zake.

“Nilinyimwa unyumba na mke wangu wiki nzima. Huku na kule baba yangu alinipigia simu kuniuliza kwa nini unachezea bahati, nikamjibu mzee sio kweli. Yanga walivyonirejesha ndipo familia yangu ikaamini sijafanya tukio hilo,” anasema Taifa.

“Baada ya kujiunga na timu, nakumbuka nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliniita na kuniambia Taita kama umefanya usirudie tena na kama hujafanya usiwaze kufanya kabisa, haya ni maisha na una familia itakuwa siyo kitu kizuri.”

Mwanaspoti linamuuliza tena unadhani kwa nini uliambiwa wewe na sio mchezaji mwingine? Anajibu: “Kwanza hadi leo sijui kesi hiyo iliisha vipi, lakini chumba ambacho nilikuwa nakaa mimi, tulikuwa na Nurdin Bakar ambaye siwezi kumsemea, labda mkamuulize kwa upande wake, ingawa zamani aliwahi kujibu aliyeshikwa na mbuzi ndio huyo huyo, iliniuma ila nikaamua kunyamaza.”  

ALIJUA HAKAI YANGA

Taita anasema mtazamo wa mashabiki wengi akiwa Yanga walimchukulia mhuni kutokana na kukulia Mburahati, Dar es Salaam hivyo mara kadhaa walikuwa wanamzomea na alijua hawezi kudumu katika kikosi.

“Kuna wanangu Yanga ilikuwa ikicheza walikuwa wanakuja kunipa sapoti. Sasa ukiwapa mfano laki ili wagawane nauli mashabiki walikuwa wanaona kama nina kundi la wahuni, nilivyoona mtazamo huo, nikajiongeza kwamba hata nikiachwa sitaona ni taarifa ngeni kwangu,” anasema Taifa aliyezaliwa Kigogo na kukulia Mburahati kabla ya kutangazwa kupitia vipaji vya soka akizichezea timu mbalimbali kama Ashanti United iliyompeleka Kagera Sugar.

Boli alilokuwa akilipiga Kagera lilimpa ulaji Yanga na kusajiliwa mwaka 2011 kabla ya kuibukia Villa Squad, kisha Majimaji Songea na baadaye kurudi Kagera Sugar, huku kwa timu ya taifa aliitwa na kuichezea mwaka 2011 akiwa Yanga.

MJENGO WA KISHUA

Akizungumza usajili wake Jangwani, anasema anashukuru ulimwezesha kupata mjengo wa maana kwa fedha alizolipwa na Yanga.

Anasema baada ya kupata dau lake la usajili la Sh19 milioni, hakutaka kucheza na pesa alimpigia simu mkewe na ndugu zake wakazichukua na kwenda kununua kiwanja na akaanza ujenzi moja kwa moja, huko Kibada, Mwasonga.

“Nimejenga nyumba nikiwa Yanga siishi kinyonge ni vile sipendi maisha yangu kuwa mtandaoni. Pia nina heka moja Kigamboni na ninafanya biashara nikisaidiana na mke wangu,” anasema.

“Jambo wasilolifahamu watu ni kwamba mke wangu tangu nilipopendana naye akiwa shule ya msingi, mimi nilikuwa kidato cha kwanza ndio maana nimeweza kudumu naye hadi leo, hivyo sikuwahi kukurupuka kwenye mahusiano, vinginevyo zile tuhuma zingeweza kutufanya tuachane. Wakati mwingine jamii nimeacha inichukulie kwa upande wa mhuni, ila sipo nilivyo, kwani mie ni baba wa familia na mume mwenye kujiheshimu mno.”

VIATU VILILETA ISHU

Taifa anasema kuna siku alikuwepo dogo mmoja mtaa wa Jangwani alikuwa anaitwa Okwii, aliingia chumbani kwake na kuchukua viatu vyake, Oscar Joshua akamuona baada ya kumbana akamtaja mchezaji aliyemtuma avichukue.

“Kama hakuna mechi nilikuwa naenda kukaa nyumbani Mburahati, Oscar alikuwa anabaki hosteli za Jangwani. Sasa akasikia mlango kwangu unafunguliwa kufuatilia akamkuta huyo dogo siwezi kumtaja nani alimtuma kuchukua viatu vyangu, maana maisha yameendelea tumekuwa wakubwa na sijui kwa sasa anafanya kitu gani huko aliko na sijui alitaka akavifanye nini, hivyo mambo ya kuibiana soksi, viatu yapo sana,” anasema.

MASTAA NA MITANDAO

Anasema wakati anacheza mitandao ya kijamii haikuwa na kasi kama sasa ndio maana waliweza kwenda bendi mbalimbali baada ya mchezo na hakukuwa na tatizo.

“Ila kwa sasa chochote wanachokifanya wajue wataanikwa kwenye mitandao ya kijamii, wanapaswa kujilinda na kujiheshimu. Hata mimi najiheshimu kupita kiasi, huwezi kunikuta nafanya vitu vya hovyo, kwani nina watoto sitaki waone wana baba asiyejielewa,” anasema nyota huyo wa zamani.

Anasema ngumi ndizo zilikuwa plani A za kumtoa kimaisha, lakini akajikuta anaangukia kwenye soka baada ya kocha Boniface Njohole (sasa marehemu) kukiona kipaji chake.

BADO ANAUTAKA

Taita anasema kitu alichokibakiza cha ndoto zake ni kupigana ngumi, kwani zamani alikuwa anafanya mazoezi zaidi kuliko mpira.

“Nimefanya mazoezi sana enzi hizo na kina bondia Thomas Mashali, Chiwa, Doto Kipenga wote ni marehemu.Hata nilipoambiwa Mashari kafariki iliniuma sana sikuwa na cha kufanya, kwani nilikuwa kambini nikiwa Kagera Sugar,” anasema Taifa.

“Kwa sasa nafanya gym maskani na wanangu kambi za Mburahati, Manzese na Mabibo, siku moja utanisikia napanda ulingoni kupigana ngumi za ushindani.”

CHAMA NA PACOME

Taifa anasema kila akiwaangalia mabeki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ namna wanavyocheza anaona wanastahili pongezi kwa kujitunza kunakowafanya hadi sasa kucheza kwa viwango vikubwa.

“Lazima tujivunie Watanzania wenzetu ambao wanafanya makubwa, si jambo dogo Kapombe na Tshabalala kulinda viwango vyao kwa mfululizo. Wamekuwa washindani mbele ya wageni ambao wamewahi kusajiliwa kwenye namba zao,” anasema.

Kwa upande wa nyota wa kigeni anaovutiwa nao anawataja Clatous Chama (Simba), Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Djigui Diarra na Khalid Aucho wa Yanga.

“Chama, Pacome na Nzengeli wanacheza kama alivyokuwa anacheza fundi Haruna Niyonzima nyakati hizo. Mwamba alikuwa anatupa burudani sana mazoezini,” anasema Taifa.

“Kwa upande wa wazawa ambao nilikuwa napenda kuangalia wakicheza alikuwa Haruna Moshi ‘Boban’, Shaaban Kisiga, Rashid Gumbo hao jamaa walikuwa na vipaji vikubwa sana, halafu hawakuwa na mambo mengi zaidi zaidi ya kugawa pasi za upendo uwanjani.”

MAFANIKIO

Nyota huyo anajivunia mafanikio mbalimbali aliyoyapata akiwa na Yanga ikiwamo kutwaa nayo mataji kadhaa mbali na kujitengenezea jina kiasi cha kuitwa timu ya taifa, japokuwa  alikutana na msala wa kutuhumiwa kuingiza uhuni kambini, japo ilibainika sio kweli.

Taita alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye kikosi kilichotwaa mataji mawili mfululizo ya Kombe la Kagame 2011 kwa kuifunga Simba bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mghana Kenneth Asamoah, kisha kutetea tena 2012 kwa kuichapa Azam mabao 2-0 mabao yaliyowekwa na Mfungaji Bora wa msimu huo, Hamis Kiiza ‘Diego’ na Said Bahanuzi, aliyetupia bao la jioni na kumpa tuzo kwa kufunga jumla ya mabao saba katika michuano hiyo.

Taita alikuwa kwenye kikosi cha Yanga kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012-2013, lakini amebaki na kumbukumbu mbaya ya kuishuhudia Yanga ikichapwa mwabao 5-0 na Simba katika mechi ya watani, kipigo kilichoondoka na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga.

Kikosi hicho cha Yanga cha msimu huo wa 2011-2012 kiliundwa na majembe haya akiwamo Taita aliyekuwa akitumika kama beki na winga wa kulia wa timu hiyo:

Makipa: Yaw Berko, Shaaban Kado na Said Mohammed ‘Nduda’, mabeki ni; Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub `Cannavaro’, Godfrey Taita, Abuu Ubwa, Bakari Mbegu, Job Ibrahim, Fred Mbuna, Salum Telela na Stephano Mwasika. Viungo: Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakar, Haruna Niyonzima `Fabregas’, Godfrey Bonny ‘Ndanje’, Rashid Gumbo, Julius Mrope na Idrissa Rashid

Washambuliaji: Kenneth Asamoah, Davies Mwape, Hamis Kizza ‘Diego’, Jerry Tegete, Pius Kisambale na Kiggi Makassy.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live