Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Beki Sakho aenda kujitafuta Georgia

Mamadou Sakho Montpellier Hsc 2023 24 1698248855 120367 Beki Sakho aenda kujitafuta Georgia

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa zamani wa Liverpool, Mamadou Sakho anajipanga kwenda kujenga upya maisha ya soka lake huko Georgia.

Beki wa kati huyo raia wa Ufaransa alitamba kwenye soka la Ligi Kuu England kwa misimu minne, aliyocheza Liverpool na Crystal Palace.

Hata hivyo, Sakho amekuwa hana timu tangu alipoachana na Montpellier kwa makubaliano ya pande mbili, Novemba mwaka jana.

Na sasa kinachoelezwa, beki huyo mwenye umri wa miaka 34 yupo kwenye mazungumzo na klabu moja ya Ligi Kuu Georgia, Torpedo Kutaisi kwa ajili ya kwenda kujiunga nayo, akipambana kurudi uwanjani na kuendelea na soka lake.

Kocha wa zamani wa Blackburn, Steve Kean, ndiye anayeinoa timu hiyo na ndiye anayemtaka Sakho ikiwa ni mpango wake katika kusajili wachezaji wenye majina makubwa ili kwenda kuboresha ubora wa kikosi chao.

Kean hakuwa maarufu sana kwa mashabiki wa Blackburn ambapo alikumbana na maandamano mengi sana kabla ya kuachana na timu hiyo 2012. Na tangu wakati huo, staa huyo wa zamani wa Swansea City, alikwenda kufanya kazi ya ukocha Singapore, Ugiriki, Australia na sasa Georgia.

Kutaisi ni jiji la tatu kwa ukubwa Georgia, nchi hiyo ipo kwenye Bahari Nyeusi na imepakana na Russia, Uturuki na Armenia.

Sakho, ambaye alisajiliwa na Liverpool kwa ada ya Pauni 18 milioni akitokea Paris Saint-Germain mwaka 2013, amepewa ofa ya mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja wa tatu na miamba hiyo ya huko Georgia.

Torpedo imempa ofa beki huyo fursa kazaa za kibiashara na bonasi kadhaa kwa familia yake pamoja na kumlipa mshahara mnono. Sakho, ambaye ameitumikia Ufaransa kwenye mechi 29, alitumikia Liverpool kwenye mechi 80 na kufunga mabao matatu.

Mzaliwa huyo wa Paris, Sakho aliichezea Palace mara 75 baada ya kujiunga nayo mwaka 2017 kisha alirudi Ufaransa kujiunga na Montpellier miaka mitatu iliyopita. Aliachana na timu hiyo ya Ligue 1 baada ya kutibuana na kocha Michel Der Zakarian.

Chanzo: Mwanaspoti