Wakati kikosi cha Namungo kikicheza mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC juzi Jumamosi nakutoka sare ya 1-1, habari njema kwa mashabiki wa timu hiyo ni kukamilisha usajili wa beki, Derrick Mukombozi kutokea Nkana Red Devils ya Zambia.
Nyota huyo raia wa Burundi alikuwa kwenye mazungumzo ya kujiunga na Tabora United na kushindwana kwenye maslahi binafsi ndipo viongozi wa Namungo wakamnasa fasta na kumpatia mkataba wa miaka miwili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaaya alisema; “Kuna wachezaji ambao bado tuko kwenye mazungumzo nao na nisingependa kuwaweka wazi hadi pale tutakapofikia makubaliano rasmi, mashabiki wetu watambue tunasajili wachezaji bora watakaokidhi matakwa yetu.”
Kaaya aliongeza sababu kubwa ya kusuasua kwenye usajili wa msimu huu ni kutokana na kufanya tathimini ya kina juu ya wachezaji wanaowaingiza kikosini kwani hawataki kuwaleta wengi ambao hawana faida kwenye timu na wanamsikiliza Kocha Cedric Kaze.
Mukombozi anakuwa mchezaji wa pili wa kigeni kusajiliwa na timu hiyo baada ya Fabrice Ngoy aliyetokea Tabora United na kuunga na nyota wengine, Erasto Nyoni (Simba), Kelvin Sabato (Polisi TZ) na Hamad Majimengi kutoka Coastal Union. Mukombozi pia amewahi kuzichezea Prisons Leopards ya Zambia na LLB Academic ya kwao Burundi.