Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Beki Mcolombia Azam amwibua Morris

Fuentes Yeison Fuentes

Fri, 7 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha wa zamani wa Azam FC, Aggrey Morris ameshindwa kujizuia kwa kuwapa tano mabosi wa klabu kwa kufanya usajili mzuri ulioibeba timu hiyo katika msimu wa mashindano wa 2023-2024 huku akimtaka beki Mcolombia, Yeison Fuentes (22) aliyemchambua na kusema amekamilika kwa kila idara.

Azam ilimsajili beki huyo wa kati kwa mkataba wa miaka mitatu, akitokea Leones FC ya Colombia na tangu ajiunge na timu hiyo ameonyesha kiwango cha hali ya juu akiibeba katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, kote ikimaliza nafasi ya pili nyuma ya wababe Yanga iliyotetea mataji hayo kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kiwango cha Fuentes kimemfanya Morris, kumwagia sifa kwa aina ya uchezaji na uwezo wa kumudu mipira ya juu, chini, kasi, maamuzi ya haraka na nguvu, vimeongeza umakini na ubora ndani ya kikosi hicho.

“Umri wake ni mdogo unaofanya awe na hamu ya mafanikio, ni beki ambaye ana kila kitu, binafsi hata baada ya sisi wengine kumaliza majukumu yetu ya ushindani uwanjani, naona wameletwa wachezaji walioziba mapengo yetu,” alisema Aggrey anayejishughulisha na ukocha kwa sasa.

“Ukiachana na Fuentes nimeona uwezo wa kipa Mohamed Mustafa, kama sikosei alikuwa kwa mkopo wa miezi sita, alitoka El Merrikh ya Sudan, kaonyesha uwezo mkubwa kama ikiwezekana viongozi wamuongezee mkataba mpya,” aliongeza Morris nahodha wa zamani wa Mafunzo aliyetua Azam mwaka juzi.

Mbali na hilo, aliipongeza Azam kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, huku ikicheza fainali ya pili mfululizo ya Kombe la Shirikisho nchini ikizidiwa ujanja na Yanga iliyobeba taji mara zote mbele yao.

“Naamini usajili unaoendelea ndani ya kikosi hicho,utakuwa na tija kubwa, kwani wataleta watu ambao watakuwa na uzoefu na michuano ya CAF,” alisema Morris, huku Kocha Mkuu wa Azam, Youssouf Dabo akimsifia beki huyo Mcolombia.

“Ni beki mzuri, kijana, anapambana kuonyesha uwezo wake, nadhani kila mtu ameona alichokifanya msimu uliopita.”

Chanzo: Mwanaspoti