IMEFICHUKA kuwa, uongozi wa Klabu ya Yanga umeingilia dili la kumnasa nahodha wa Biashara United, Abulmajid Mangalo ambaye amekuwa akiwindwa kwa ukaribu na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba.
Hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, aliwasilisha ripoti ya usajili ambapo miongoni mwa maeneo ambayo amehitaji yafanyiwe maboreshio ni nafasi ya mlinzi wa kati akitaka bonge la beki kuja kuwapa changamoto, Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.
Mpaka sasa Mangalo amebakisha mkataba wa miezi saba ndani ya Biashara United, huku baadhi ya timu zikiwemo Simba na Yanga zikipigana vikumbo kumnasa nahodha huyo.
Mangalo alisema: “Ni kweli kumekuwa na mawasiliano kati ya uongozi unaonisimamia na baadhi ya viongozi wa Yanga, ambao wameulizia uwezekano wa kunisajili, lakini bado mazungumzo hayo yapo katika hatua za awali.
“Mkataba wangu na Biashara kwa sasa umesaliwa na muda wa miezi saba, kuna timu mbalimbali ambazo zimeonesha nia ya kunihitaji, kama mchezaji niko tayari kwa ajili ya changamoto mpya na ikiwa kuna timu ambayo itafikia makubaliano na Uongozi wangu na wa Biashara United basi niko tayari kusaini.