Siku chache sana zimebaki kuumaliza mwaka wa 2021. Na hakika huu ni mwaka ambao baadhi ya wachezaji wanapenda upite tu.
Kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, kuna wanasoka kibao wameshuhudia thamani zao zikishuka sokoni, lakini kuna baadhi hao, zimeporomoka kwa kiwango kikubwa kuliko maelezo.
Kwa mujibu wa Transfermarkt, hii hapa orodha ya mastaa matata kabisa ambao thamani zao zimeshuka kwa kiwango kikubwa sana sokoni mwaka huu wa 2021.
Kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak thamani yake ya sasa sokoni ni Euro 70 milioni, lakini hiyo imeshuka kwa Euro 20 milioni. Kipa huyo raia wa Slovenia, amekuwa kwenye kiwango bora - lakini thamani yake sokoni imeshuka kwa Euro 20 milioni.
Beki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold ni moja ya wachezaji ambao pia thamani yake imeshuka kwa kiwango kikubwa, ambapo kwa sasa thamani yake sokoni ni Euro 75 milioni, ikiwa imeshuka kwa Euro 35 milioni.
Mkali wa Barcelona, Clement Lenglet thamani yake ya sokoni kwa sasa ni Euro 18 milioni, lakini ikiwa imeshuka kwa Euro 32 milioni kwa mwaka huu, huku beki kisiki kabisa wa Liverpool, Virgil van Dijk - aliyesajiliwa kwa pesa nyingi, thamani yake ya soka kwa sasa ni Euro 55 milioni, lakini kiwango hicho kimeshuka kwa Euro 25 milioni kwa mwaka huu. Jambo kubwa lililomshusha thamani Van Dijk ni majeraha.
Kiungo mkabaji, Miralem Pjanic ni staa mwingine ambaye thamani yake sokoni imeshuka kwa kiwango kikubwa, Euro 32 milioni na hivyo kumfanya awe na thamani ya Euro 18 milioni tu sokoni kwa sasa. Uhamisho wa Pjanic kwenda Barcelona uliishia kuwa majanga tu na tayari unachunguzwa kuwa kati ya sajili za magumashi ambazo Juventus wamekuwa wakifanya kwa kuwapandisha wachezaji wao thamani isiyostahili.
Chelsea ilinasa huduma ya Saul Niguez kwa mkopo kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi akitokea Atletico Madrid ni miongoni mwa mastaa ambao thamani zao zimeporomoka sokoni, ikishuka kwa Euro 30 milioni na kumfanya awe na thamani ya Euro 40 milioni tu sokoni kwa sasa.
Staa wa Kibrazili, Phili-ppe Coutinho amekuwa na wakati mgumu huko Barcelona, kukaa benchi kumeshusha thamani yake kwa kiwango kikubwa sana, ikiporomoka kwa Euro 40 milioni na hivyo kumfanya awe na thamani ya Euro 20 milioni tu sokoni kwa sasa.
Sawa, kwa wakati huu ukihitaji saini ya Mohamed Salah lazima ujipange, akitajwa kuwa na thamani ya Euro 100 milioni sokoni, lakini kiwango hicho kimedaiwa kwamba kushuka kwa Euro 20 milioni, ambapo thamani halisi ya mkali huyo wa Liverpool ni Euro 120 milioni.
Sadio Mane ni mchezaji mwingine ambaye thamani yake sokoni imeshuka kwa Euro 35 milioni na kumfanya awe na thamani ya Euro 85 milioni huko sokoni ukihitaji huduma yake kwa kuzingatia Transfermarkt.
Kikosi cha Jurgen Klopp cha Liverpool yenye maskani yake huko Anfield kinaonekana mastaa wake wengi thamani zao kushuka huko sokoni kwa mwaka 2021, ambapo straika Roberto Firmino, naye aliporomoka kwa Euro 32 milioni na kumfanya Mbrazili huyo awe na thamani ya Euro 40 milioni tu kwa sasa. Majeraha na ujio wa Diogo Jota huko Anfield umemfanya Firmino kuwa na wakati mgumu wa kupata namba.