Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bayo: Wanaopinga uongozi wangu RT hawajui watendalo

Bayo Pic Data Bayo: Wanaopinga uongozi wangu RT hawajui watendalo

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Siku kadhaa baada ya kuibuka taarifa za kupingwa kuwa makamu wa rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), John Bayo amesema walioibua mjadara huo hawajui watendalo.

Bayo alichaguliwa miezi kadhaa iliyopita kwenye uchaguzi mkuu wa RT kuwa makamu wa rais akichukua nafasi ya William Kalaghe aliyeondolewa kwenye usaili usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi.

Akiwa madarakani, mmoja wa wadau aliyejitambulisha kuwa ni Johnson Maganga aliandika barua kwenda wizara ya michezo akilalamika kuwepo na uvunjifu wa katiba kuhusu elimu ya Bayo.

Alidai katiba ya RT inataka rais na makamu wa raisĀ  kuwa na elimu kuanzisa Stashahada na Bayo hana elimu hiyo.

Akijibu mapigo, Bayo amesema watu walioanzisha 'zengwe' hilo dhidi yake anawafahamu na amewasamehee kwani hawajui walitendalo.

"Wanasema sina Stashahada, walete ushahidi na kama kweli huyo Johnson Maganga anaamini asemacho ajitokeze hadharani ili tupambane kwa hoja.

"Nawafahamu walioanzisha sekeseke hilo, wako wanne (aliwataja majina), wameamua kutumia jina la Johnson Maganga ili kuvuruga tu ila hawajui watendalo," amesema.

Amesema yeye amesoma kwenye moja ya vyuo kilichopo Namanga, mpakani mwa Kenya na Tanzania.

"Nikiwa nasoma sio kila mtu afahamu, ila nimesoma Namanga na kuhitimu huko na ushahidi wa vyeti upo, lakini baadhi ya watu wameona uongozi wetu umeanza vizuri RT wanaibua migogoro ambayo binafsi naona haina tija katika ustawi wa riadha ya Tanzania.

"Muda ambao wanatumia kuibua haya tungeshirikiana kuandaa timu kwa ajili ya Olimpiki, bila shaka tungefika mbali, ila narudia tena kusisitiza walionianzishia zengwe nimeshawafahamu ni watu ambao tuko nao hapa Arusha na wanafanya hivi kwa sababu binafsi," amesema.

Kuhusu kusoma, Bayo alisema yeye ana vyeti ambavyo vimeandikwa majina yake halisi ya John Gilbert Bayo.

"Nina kijana wangu anaitwa Gilbert John Bayo, katika kuunganisha 'dot' ndiyo wanasema kwamba yeye ndiye amesoma na si mimi, hivi kwani nikitaka kusoma nawaaga wao au?.

"Niligombea RT nikijua na sifa zote za kuwa kiongozi ambazo katiba ya Shirikisho imezianisha, wenye wasiwasi na elimu yangu wasubiri kuletewa ushahidi itakapobidi," amesema.

Akizungumzia safari ya uongozi wao tangu walipokabidhiwa kijiti, Bayo amesema licha ya kuingia na kukuta changamoto ya ukata, lakini wameendelea kupambana nayo.

"Tuliachiwa ofisi akaunti ya kwanza ikiwa na Sh 108,000 na ya pili ikiwa na Sh 46300, wakati huo huo Shirikisho likiwa na madeni na mishahara ya wafanyakazi haijalipwa, lakini tumepambana navyo na timu imeingia kambini kujiandaa na Olimpiki licha ya ukata unaotukabiri,".

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz