Mabosi wa Bayern Munich wamepanga kuingia kwenye mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Liverpool, Fabinho ikiwa dili lake la kujiunga na Al Ittihad litafeli.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Sports hadi sasa bado Ittihad haijafikia muafaka na Liverpool juu ya mauzo ya Fabinho hali ambayo inaonyesha dili hilo huenda likafeli.
Mabosi wa timu zote hizi wamepanga kufikia makubaliano ya kukamilisha dili la Fabinho kutua Saudi Arabia kabla ya wiki hii haijamalizika lakini hadi sasa mambo yanaonekana kuwa magumu. Inaelezwa Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel anahitaji sana huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Brazil kutokana na aina ya uchezaji wake.
Fabinho amebakiza miaka mitatu katika mkataba wake Liverpool, kumaanisha kuwa klabu yake iko kwenye nafasi nzuri ya kufanya mazungumzo na huenda ikafanya biashara na timu itakayotoa dau zuri ambalo litaishawishi kwa kuongeza bei ya uhamisho.