Bayrn Munich imeripotiwa kuwa na mpango wa kwenda kuvamia Manchester United kunasa saini ya Bruno Fernandes.
Kiungo huyo Mreno alidai kwamba hatima ya maisha yake huko Old Trafford imekuwa kwenye hali ya sintofahamu na kutishia kuondoka endapo kama Man United itashindwa kufanya usajili wa nguvu wa kuleta mastaa wa maana kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Fernandes, 29, alichaguliwa kuwa nahodha wa Man United na kocha Erik ten Hag, mwaka jana, lakini sasa anashawishika na mpango wa kuondoka.
Na Bayern imeanzisha mazungumzo na wakala wake, Miguel Pinho kwa ajili ya kunasa saini yake kwenye dirisha hili, kwa mujibu wa O Jogo.
Ripoti hizo zinabainisha zaidi kwamba Barcelona ni timu nyingine inayohitaji saini ya kiungo huyo wa Kireno, Fernandes. Fernandes amedumu kwenye kikosi cha Man United kwa kipindi cha miaka minne na nusu.
Na hivi karibuni Fernandes alisema kwamba baada ya fainali za Euro 2024 atatoa msimamo wake kama atahitaji kwenda kukabiliana na changamoto mpya kwingineko. Kwa msimu huu, Man United imeshinda taji la Kombe la FA na hivyo msimu ujao itacheza kwenye Europa League.
Fernandes alisema: “Ninachotaka ni klabu kuendana na mipango yangu. Kama ukienda kuzungumza na shabiki yeyote, atakwambia kitu hicho hicho. Tunataka kuwa washindaji kwenye ligi. Tunataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, tunataka kufike fainali za makombe. Hiyo ndiyo levo yetu inayotufaa. Hicho ndicho ninachotaka. Ndicho tunachostahili.”
Bayern itavamia kunasa mastaa wenye vipaji kwenye Ligi Kuu England baada ya kuteua Vincent Kompany kuwa kocha wao mpya, huku tayari kwenye kikosi hicho cha Allianz Arena kuna mastaa wawili waliokuwa moto kabisa kwenye ligi ya England, Harry Kane na Eric Dier.