Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich Oliver Kahn amethibitisha kwamba wababe hao wa Bavaria hawatakuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania saini ya Erling Haaland mwaka ujao.
Mabingwa hao wa Bundesliga ni moja kati ya timu zinazotajwa zaidi kuisaka saini ya mchezaji huyo wa Borussia Dortmund wakati kipengele chake cha kuachiliwa kitakapoanza kutumika msimu wa joto.
Bayern wanakabiliwa na sintofahamu kuhusu mustakabali wa mshambuliaji nyota wa sasa Robert Lewandowski, lakini Kahn hatarajii mchezaji huyo wa kimataifa wa Poland kuondoka hivi karibuni.
Kahn akizungumza na Suddeutsche Zeitung alisema “Tunaye Robert Lewandowski. Atafunga mabao 30 au 40 zaidi kwa miaka kadhaa ijayo.” baada ya kuulizwa mipango yao juu ya Erling Braut Haaland
Kutokana na hali hiyo, Manchester United, Barcelona, Paris Saint-Germain, Real Madrid na Manchester City wanapunguziwa ushindani kumpata Haaland, huku timu hizo zikisemekana zinataka kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Norway mwaka ujao.
Haaland amefikisha mabao 76 katika michezo 75 pekee ya Dortmund kwenye mashindano yote, ikijumuisha mabao 19 kutoka mechi 16 za kampeni ya 2021-22.