Klabu ya Manchester City imeliita tukio la kushambuliwa kwa basi la wachezaji wa Liverpool kuwa ni kitendo 'kisichokubalika' katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya klabu hiyo.
Kikosi cha Pep Guardiola kiliibuka na ushindi wa 4-1 dhidi ya mahasimu wao shukrani kwa mabao ya Julian Alvarez, Kevin De Bruyne, Jack Grealish na Ilkay Gundogan.
Hata hivyo, ushindi huo ulipakwa tope na taarifa kwamba basi la wachezaji wa Liverpool liliharibiwa wakati likiondoka kutoka kwenye Uwanja wa Etihad Jumamosi jioni.
Polisi wa Greater Manchester wamethibitisha kwamba wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo la kihalifu.
"Tunafahamu kwamba tofali lilirushwa kutoka katika eneo la makazi ya watu. "Matukio kama haya hayakubaliki hata kidogo, na tunakemea vikali. "Tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika upelelezi wa polisi wa Greater Manchester kuhusu tukio hili."
Man City pia ilieleza kutofurahishwa na nyimbo zisizo za kiungwana zilizokuwa zikiimbwa na mashabiki wake dhidi ya Liverpool wakati wa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Etihad.