Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barua nzito kwa mastaa Bongo

Kibu X Diarra Faini Barua nzito kwa mastaa Bongo

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) yanamalizika siku chache zijazo. Leo kinapigwa michezo miwili ya nusu fainali na baadaye usiku tutajua ni kina nani wanaangukia katika kusaka tatu bora ya kipute hicho na wale watakaokiwasha katika fainali itakayopigwa Jumapili ijayo, Februari 11 jijini Abidjan, Ivory Coast.

Kuna timu nne zimetinga nusu fainali hizo za 34 za Afcon ambazo ni DR Congo, Ivory Coast, Nigeria na Afrika Kusini na ndizo zinazokiwasha baadaye leo saa 2:00 na saa 5:00 usiku. Mengi yameelezwa, yamesimuliwa na hata kuandikwa kuhusu mashindano hayo ambayo yameuweka rehani utawala wa nchi zilizofahamika kama vigogo vya soka Afrika, baada ya mataifa mengi kuondolewa katika hatua mbalimbali za mashindano hayo.

Hakuna aliyetarajia ingekosekana hata nchi moja katika nusu fainali kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Afrika. Nani alitarajia kuikosa Morocco inayoshika nafasi ya 13 kwa ubora wa kandanda duniani ikiziacha kwa mbali nchi kama Ujerumani, Mexico, Denrmark na Uswisi.

Yaani kweli Morocco hii iliyoandika historia mpya baada ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia kule Qatar mwaka 2022, imeshindwa kuingia nusu fainali ya Afcon 2023!!?

Hivi nani hakuitarajia Senegal iliyosheheni mastaa wakubwa duniani ikiikosa walau nusu fainali tu ilhali ina nyota kibao wanaocheza Ulaya na wana majina makubwa katika klabu wanazochezea, lakini pia ikiwa ni nchi ya 20 kwa ubora wa soka duniani ikizitimulia vumbi nchi kubwa kisoka kama Ukraine na nyinginezo?

Jibu ni jepesi tu, mpira umebadilika na lolote linawezekana uwanjani. Kila nchi imepiga hatua kisoka hata kama mashindano inayoandaa ndani bado yapo nyuma. Waswahili wanasema kwamba mpira unadunda na ndiyo maana una maajabu yake. Haya ya miaka ya hivi karibuni ndio maajabu halisi ya soka.

Fikiria juu ya matokeo ya kushangaza ya Afcon mwaka huu ambapo nchi zinazofahamika kama vigogo vya soka zimeshindwa hata kupata tu ushindi mbele ya mataifa yanayojulikana kama machanga katika mchezo huo. Fikiria juu ya aibu ambayo mastaa wakubwa duniani kutoka Afrika walivyoshindwa kuzibeba nchi zao walau hata kwa kufunga bao katika mashindano hayo.

Hii ndio maana halisi ya mabadiliko makubwa ya soka. Hii ndio maana inayoonyesha kwamba kumbe hata mastaa wa Kitanzania wanapaswa kutokata tamaa, badala yake waendelee kupambana wakiamini kwamba ndoto za mafanikio yao na nchi kwa ujumla wanatembea nazo mikononi mwao.

Kama Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto na Mohammed Hussein 'Tshabalala' waliweza kuwazuia nyota kibao wanaocheza Ulaya na kuwatoa jasho kule Ivory Coast, nini kinashindikana kwa mastaa hawa wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kukomaa na kufika mbali ikiwamo kucheza soka huko Ulaya wanakocheza hao waliowabana?

Pengine kilicho wazi kwao na ambacho wanapaswa kuendelea kupambana nacho ni kuondokana na hofu pale wanapokabiliana na nyota wenye majina makubwa, kwani hiyo ndiyo inayowatesa wachezaji wengi kutoka katika nchi kama zetu.

Nyota hawa mara nyingi hofu yao inakimbilia kuamini kwamba mtu kama Mohamed Salah au

Victor Osimhen anapotajwa na kuandikwa kuwa na maajabu mengi uwanjani, basi hata kukabiliana naye inakuwa vivyo hivyo kwamba ni kama haiwezekani.

Badala ya kujiuliza kwamba, ni wachezaji wangapi ambao katika historia ya maisha yao ya soka wamemkabili Messi na Ronaldo na hakuleta madhara katika timu zao.

Wakati mafanikio ya timu ndogo katika Afcon mwaka huu yakibaki kuwa kioo cha siku za usoni kwa nchi hizo, ni vyema sasa tukakichukua kioo hicho na kuanza kujiangalia kwacho. Kwamba mpira wa Afrika kupitia programu mbalimbali hasa zile za maendeleo ya ufundi, vijana na miundombinu zinaanza kuzaa matunda? Ndio na ni vyema serikali na Shirikisho la Soka (TFF) wakashikilia hapohapo ili kuibua vipaji vingi vipya.

Kwamba tofauti ya kiuwezo kwa wachezaji wanaocheza nje ya Afrika na wanaocheza nyumbani inazidi kupungua? Ndio, na nyota wa Taifa Stars wanapaswa kuamini hivyo na wanapokabiliana nao uwanjani wasiwahofie kiviiile.

Kwamba wachezaji wanaocheza Ulaya hawaweki juhudi zote wanapotumikia timu za taifa? Maswali ni mengi, lakini kubwa viwango vyao licha ya kwamba wanatumia miundombonu bora zaidi ni vile vinavyoshindanika na vikabika na kupigika.

Chanzo: Mwanaspoti