Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baresi sasa kiroho safi Prisons

TANZANIA PRISONS.png Baresi sasa kiroho safi Prisons

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Matokeo ya ushindi katika mechi mbili mfululizo yameongeza morali na mzuka kwa Tanzania Prisons, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ akitangaza mkakati wa kumaliza salama ligi kuu katika nafasi nzuri, huku mastaa nao wakiahidi makubwa.

Prisons ambayo haikuwa na mwanzo mzuri hadi kufikia hatua ya kumtimua aliyekuwa kocha wake Patrick Odhiambo, kwa sasa imeonekana kuamka upya na kujinasua nafasi za mkiani.

Katika mechi mbili zilizopita, ‘Wajelajela’ hao walishinda dhidi ya Nmaungo ugenini 3-2 kisha kuibanjua Polisi Tanzania 3-0 na kupanda hadi nafasi ya 10 kwa pointi 28.

Timu hiyo ya jijini hapa imebakiza mechi nne dhidi ya Geita Gold, Kagera Sugar, (ugenini) kisha nyumbani kucheza na KMC na kuhitimisha msimu dhidi ya Yanga.

Baresi alisema matokeo hayo yameleta mabadiliko chanya kikosini kwa kila mmoja kuonesha ari na kufanya kuwa na matumaini ya kuendeleza ushindi na kumaliza ligi nafasi nzuri.

“Tunaendelea na mazoezi kujiandaa na mechi mbili za ugenini, tunahitaji alama sita katika michezo hiyo kabla ya kurudi nyumbani ili kumaliza ligi nafasi nzuri hatutaki play off wala kushuka daraja,” alisema Baresi.

Nahodha wa timu hiyo, Benjamin Asukile alisema licha ya ugumu na ushindani ulivyo kwa timu za kushuka daraja, Prisons iko makini kuhakikisha haiachi kitu katika mechi zilizobaki.

“Kikubwa mashabiki waendelee kutuombea na kutusapoti, vita ni ngumu ila hatuwezi kubweteka kwa sababu safari bado ni nzito, lazima tupambane kadri ya uwezo tushinde mechi zilizobaki,” alisema Asukile.

Chanzo: Mwanaspoti