Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baresi kuisoma Simba ikiwa Cairo

Baresi Muda Baresi kuisoma Simba ikiwa Cairo

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashujaa imesema itakuwa makini kufuatilia mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly na Simba inayopigwa kesho Ijumaa saa 5:00 usiku ili kujua wapi pakupitia watakapokutana na Wekundu wa Msimbazi katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC).

Simba itakuwa uwanjani jijini Cairo, Misri kurudiana na Al Ahly baada ya kupoteza Kwa Mkapa kwa bao 1-0 ili kusaka tiketi ya kwenda nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

Mara baada ya mchezo huo, Simba inarudia nyumbani na moja kwa moja kuifuata Mashujaa mjini Kigoma katika mechi ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC) utakaochezwa Aprili 9 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Mashujaa licha ya kutamba kuishangaza Simba, lakini wanakutana na vigogo hao wakiwa haijapata ushindi wala sare kwao katika michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu wakifungwa zote.

Hata hivyo, Maafande hao wanajivunia rekodi waliyowahi kufanya msimu wa 2020/21 walipoifunga Simba katika michuano hiyo mabao 3-2 hatua ya 32, mechi ikipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika ikiwa chini ya Kocha Atuga Manyundo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ alisema kwa sasa wanaendelea kujifua wakihitaji kufuta uteja na kufuzu robo fainali ya kombe hilo akisema watakuwa makini kuangalia udhaifu wao.

Alisema wanaifahamu mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na ubora na uzoefu ilionao Simba kwani watakuwa wametoka kwenye mechi za kimataifa, hivyo watakuwa makini kukabiliana nao.

“Huu ni mchezo wa mtoano, lazima timu iingie uwanjani kwa kushambulia mwanzo mwisho, wamtufunga mechi zote za Ligi Kuu, hivyo sehemu ya kulipiza ni hapa Shirikisho,” alisema Batresi na kuongeza;

“Tutakuwa makini kuwaangalia kujua wapi tutapitia, tutawaheshimu kwa ukubwa wao, lakini hatutawaogopa, tunahitaji nafasi ya robo, nusu hadi fainali.”

Katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo, Simba ilishinda 1-0 mjini Kigoma likitupiwa kwa penalti na Saido Ntuibazonkiza na ikashinda tena jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0 mabao yote yakifungwa na Clatous Chama.

Chanzo: Mwanaspoti