Beki wa Mashujaa, Omary Kindamba amemmwagia sifa kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Bares’ kuwa ni zaidi ya mzazi kutokana na kuishi vizuri na wachezaji.
Mashujaa baada ya kucheza mechi tatu inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi saba na haijapoteza mechi yoyote nyumbani.
Tangu Mashujaa imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu ilianza na Kagera Sugar kwa ushindi wa mabao 2-0, kisha suluhu na Geita Gold, na dhidi ya Ihefu ikaondoka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.
Kindamba alisema wamekuwa na kocha huyo kwa muda mfupi, lakini huishi na wachezaji vizuri ndio siri ya ushindi mkubwa.
Aliongeza kuwa matokeo hayo yamekuwa mwanzo mzuri kwao na watapambana kuhakikisha wanafanikisha lengo la timu.
“Tunashukuru Mungu umekuwa mwanzo mzuri kwetu ligi ni ngumu sana na kadri muda unavyozidi kwenda ndio inaendelea kuchangamka na siri kubwa ya ushindi wetu ni kocha Baresi ambaye amekuwa nasi kama mzazi au zaidi huku akituelekeza mambo mapya kila mara,” alisema Kindamba.