Kimeeleweka. Ndivyo unaweza kusema kuelezea dili la aliyekuwa kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Abadlah Mohamed 'Baresi' kumalizana na Mashujaa FC kwa ajili ya msimu ujao.
Licha ya viongozi wa Prisons kutofafanua kwa undani kuachana na kocha huyo, lakini Mwanaspoti imelezwa kuwa Baresi na Mashujaa kimeeleweka na muda wowote atatangazwa.
Kocha huyo aliyeiachia mafanikio Prisons kwa muda mfupi, amesema licha Wajelajela hao kutamani kubaki naye lakini ishu ya maslahi imekuwa changamoto kwa kile alichohitaji na sasa ameomba kutafuta maisha mapya.
"Ni kweli uelekeo ni huko mwisho wa reli kwa sababu wamenihitaji, japo ofa zipo nyingi, Prisons walitaka niendelee kuwepo ila maslahi ni kidogo lakini nashukuru kwa ushirikiano wao hata siku nyingine tutafanya kazi" amesema Baresi.
Mashujaa inatarajia kushiriki ligi kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja kipitia play off ilipowatoa Mbeya City iliyokuwa ligi kuu kwa jumla ya mabao 4-1.