Hali ya kikosi cha Tanzania Prisons imezidi kuwa ngumu baada ya kichapo cha bao 1-0 mbele ya Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika, Moshi.
Kichapo hicho kinaifanya Prisons kuzidi kuwa katika wakati mgumu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu inayoelekea ukingoni kwa kushika nafasi ya 14 ikiwa na alama 22 sawa na Coastal Union.
Prisons wiki hii itakuwa Mkwakwani Tanga kucheza na Coastal Union ambayo imetoka kuisambaratisha Mbeya City katika uwanja huo.
Kocha wa Tanzania Prisons, Mohamed Abdallah 'Bares' amezidi kujiweka pabaya tangu ameipokea timu hiyo mikononi mwa Patrick Odhiambo ameiongoza katika michezo miwili akitoa sare dhidi ya Mtibwa kisha kulala kwa Polisi.
"Tumepambana sana, tumepata nafasi nyingi lakini mwisho wa siku tumepoteza mchezo kitu ambacho sio kizuri sababu vijana hawakuwa makini kutumia nafasi tulizokuwa tukizipata.
"Kumekuwa na tatizo la kujirudia kila wakati na kuyafanyia kazi uwanja wa mazoezi lakini kumekuwa na tatizo la umakini kwa mchezaji," alisema kocha msaidizi wa Prisons, Shabaan Mtupa.
Aliongeza bado nafasi ipo ya kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu sababu wanamichezo mingine ambayo wakipata ushindi wanaweza kutoka eneo la hatari.
Michezo mingine iliyosalia kwa Tanzania Prisons ni dhidi ya Namungo, Ruvu Shooting, Geita Gold, Kagera Sugar, KMC kisha itafunga msimu dhidi ya Yanga Uwanja wa Sokoine.
Msimu uliopita Prisons ilinusurika kushuka daraja baada ya kucheza hatua ya mtoano na Mtibwa Sugar na kuchapwa na kukutana na JKT Tanzania hatua ya mwisho ya mtoano ambapo ilifanikiwa kubaki Ligi Kuu.
Ushindi wa juzi unaifanya Polisi Tanzania kutoka mkiani na kufikisha alama 17 na sasa Ruvu Shooting ikishuka mkiani kwa alama zake 16.