Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed 'Baresi' amesema sababu kubwa ya timu yake kufungwa mabao 4-1 na kutolewa 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Yanga imechangiwa na kadi nyekundu.
Katika mchezo huo wa 16 bora uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi juzi, Prisons ilicheza pungufu dakika zote 45 za kipindi cha pili kufuatia beki, Ibrahim Abraham kutolewa nje baada ya kumfanyia madhambi Tuisila Kisinda.
"Tulianza mchezo vizuri lakini baada ya kadi nyekundu uliona tulikuwa na mlima mrefu hususani unapocheza na timu yenye wachezaji bora kama Yanga, binafsi tumeumia kwa sababu tulikuwa na uwezo pia wa kufanya makubwa." Baresi aliongeza baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo akili zao sasa watazielekeza katika michezo ya Ligi Kuu Bara.
"Tumebakiwa na shindano moja tu hivyo tunahitaji kuweka nguvu za ziada kwa sababu hatuko kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo, huu ni wakati mzuri kwetu na wachezaji kuangalia jinsi gani tunarudi tukiwa imara," alisema Baresi aliyeipa Mlandege ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2023.
Prisons ilifika hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya Mashujaa inayoshiriki Championship kwa penalti 8-7 baada ya mchezo huo kuisha suluhu.