Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema Kagera Sugar itakuwa katika wakati mgumu tofauti na mechi mbili zilizopita walipocheza dhidi ya Young Africans na Singida United katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kagera Sugar itawaalika Mashujaa kesho Ijumaa (Februari 16) kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani, Kagera.
Bares ameikumbusha Kagera Sugar wao ni timu tofauti na wamejipanga kushuka dimbani wakiwa na mbinu mbadala.
Kocha huyo amesema amewataka wachezaji wake kuongeza utulivu katika mechi hiyo ya kwanza ya mzunguko wa pili ili kuvuna Pointi tatu muhimu.
“Kagera Sugar imekuwa na matokeo mazuri siku za hivi karibuni na watataka kuendeleza, na sisi tumetoka kwenye matokeo ambayo si mabaya sana, tutakachohakikisha ni kucheza kwa nidhamu, wachezaji wetu watapaswa kujituma na kuhakikisha tunaondoka na ushindi ili hata kama hatutatoka sana chini ya msimamo lakini kutakuwa na uwelekeo mzuri wa kwenda juu.” ametamba Bares.
Kocha huyo amekiri timu yake iko katika nafasi mbaya kwenye msimamo, hivyo anataka kuona wanajiondoa katika nafasi hiyo kwa kupata ushindi au kugawana Pointi.
Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo Alhamis (Februari 15) kwa JKT Tanzania kuwakaribisha Simba SC kwenye Uwanja wa Jenerali Isamhuyo ulioko Mbweni, Dar es salaam.