Tanzania Prisons imelazimishwa suluhu nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Ijumaa, Februari 3 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mchezo huo ulikua wa kwanza kwa kocha wa Tanzania Prisons, Mohamed Abdalah 'Bares' ambaye amechukua mikoba ya Patrick Odhiambo aliyetimuliwa Januari 22 mwaka huu.
Chukua hii Mtibwa Sugar katika michezo 11 ya ugenini msimu huu haijashinda mchezo wowote kwenye ligi.
Walima miwa hao wenye alama 26 imepoteza michezo saba huku minne ikitoa sare na mara ya mwisho kuambulia alama ugenini kabla ya mchezo huo wa Prisons ilikuwa Desemba 20 mwaka jana ilipotoka suluhu na Ruvu Shooting.
Mtibwa imekuwa vizuri zaidi nyumbani ambapo katika michezo 11 imeshinda michezo mitano, sare nne na kupoteza michezo miwili dhidi ya Yanga (1-0) kisha ikalala mbele ya Azam FC kwa kichapo cha mabao 4-3.
Msimu uliopita timu hizi zilinusurika kusuka daraja baada ya kumaliza msimu, Mtibwa ikiwa nafasi ya 13 kwa alama 31 huku Prisons nafasi ya 14 kwa alama 29 na kukutana hatua ya mtoano.
Kuanzia mwaka 2015 zimekutana kwenye Ligi Kuu mara 16, Mtibwa ikishinda mara tatu na mara zote ikiwa nyumbani huku sare ikiwa michezo 10 na Prisons imeshinda michezo mitatu.
Tanzania Prisons mara ya mwisho kupata ushindi ilikua Desemba 25 mwaka jana ilipoichapa Mbeya City mabao 2-1