Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Barcelona yashindwa kutumia fursa

Barcelonaaaaaaaaaaaa Barcelona yashindwa kutumia fursa

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Barcelona imeshindwa yenyewe buana kutumia faida ya wapinzani wake kuteleza kwenye La Liga baada ya kutoka sare tasa dhidi ya Athletic Bilbao jambo ambalo limewafanya kuendelea kusalia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.

Wakati ikionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, Barcelona ilijikuta na kipindi kigumu baada ya wenyeji wao kucheza kwa kujilinda zaidi. Kati ya nafasi nzuri ambazo Barcelona ilizipata ilikuwa ni pamoja na ile Cancelo lakini uimara wa Yeray Alvarez uliifanya Bilbao kuwa salama.

Huku Girona inayoshika nafasi ya pili ikipoteza dhidi ya Mallorca, ushindi wa Barcelona ungewafanya wasogee hadi nafasi ya pili. Mpango wa Athletic ulifanya kazi kwa uhakika, na kuwanyima Barcelona nafasi za wazi.

Mbali na Barcelona kuwa na wakati mgumu kimchezo, Xavi alionekana kuwa na hofu juu ya nyota wake wawili, Frenkie de Jong na Pedri kutokana na mbele yao kuwa na mchezo wa marudiano katika hatua ya 16 bora dhidi ya Napoli.

Sare ya mabao 2-2 ya Real Madrid dhidi ya Valencia Jumamosi iliwapa Barcelona matumaini ya kupunguza pengo kileleni hadi pointi sita pekee. Kwa sasa sare hiyo haina faida kwa pande zote mbili huku Barcelona wakisalia nafasi ya tatu huku pointi zikiendelea kusalia nane nyuma ya Real Madrid. Athletic Bilbao walio katika nafasi ya tano wameshuka kwa kasi mbali na nafasi nne za juu kwenye msimamo huku wakiwa pointi tano nyuma ya Atletico Madrid, ambao waliwafunga Real Betis kwa mabao 2-1.

MSIKIE XAVI

“Lazima tujikosoe. Ilikuwa ni fursa nzuri iliyopotea. Sina hisia nzuri juu ya namna ambavyo tumeshindwa kufanikisha kile ambacho tulikuwa tumekilenga, ninaondoka nikiwa nimekata tamaa,” alisema katika mkutano na waandishi wa habari. Xavi pia alikiri kwamba “majeraha labda yametuathiri”, akimaanisha yale ya Frenkie de Jong na Pedri, kwa sababu “ni wachezaji wawili wenye uamuzi wa mambo makubwa”. “Wao ndio wanaoipa timu haiba katika safu ya kati,” alisema, akitumai kuwa “muda wa kupona katika matukio mawili utakuwa mdogo kuliko ilivyotarajiwa”.

Ubaguzi wa Vinicius kuchunguzwa

La Liga inachambua video inayoripotiwa kuonyesha nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr akifanyiwa kitendo cha ubaguzi wa rangi wakati timu hiyo ikicheza huko Valencia. Video hiyo iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii inadaiwa inaonyesha shabiki mtoto akimbagua mchezaji huyo, linaripoti The Athletic.

Vinicius alifunga mara mbili katika sare ya mabao 2-2 Jumamosi na akashangilia kwa kuinua ngumi hewani. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekabiliwa na unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi mara kadhaa huko Hispania ambako anacheza soka la kulipwa. Mei 2023, Vinicius alisema “La Liga ni ya wabaguzi wa rangi” baada ya kubaguliwa na mashabiki wa Valencia huko Mestalla.

Watu watatu baadaye walikamatwa kuhusiana na unyanyasaji huo na Valencia walitozwa faini na kuamriwa kufunga uwanja wao kwa mechi tano, baadaye kupunguzwa hadi tatu baada ya kukata rufaa. Unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi ambao Vinicius amekabiliana nao katika miezi 18 iliyopita ni pamoja na Septemba 2022 - Baadhi ya mashabiki wa Atletico Madrid waliimba nyimbo za ubaguzi wa rangi kwa Vinicius nje ya uwanja wao wa Metropolitano.

Morata apewa maua yake

Kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone amefurahishwa na ushindi dhidi ya Real Betis siku ya Jumapili. Atletico ilishinda 2-1 huku Alvaro Morata akifunga bao la ushindi. Baadaye Simeone alisema: “Tulitoka kwenye mchezo mgumu, juzi hatukuweza kufika fainali, jambo ambalo tulilitaka kwa ari kubwa, watu wetu (mashabiki) walituunga mkono wakati wote licha ya matokeo ambayo hatukuweza kuwapa Alhamisi.

“Tulianza mchezo vizuri sana huku tukiwa na umiliki mkubwa lakini wapinzani wetu waliimarika, wakati matokeo yakiwa 2-1 presha ilikuwa kubwa kwetu na hofu, kila kitu kinachozunguka kwa watu hasi na kwa bahati nzuri kuna watu chanya zaidi. Kuhusu Morata, alisema:

“Nilichogundua ni wastani mzuri wa mabao alionao kwenye soka lake na anaenda kufanya zaidi, ataendelea kuboresha namba hizi, ni muhimu sana. Natumai atatupeleka kuelekea katika kile tunachotaka. Nilivutiwa pia na Memphis Depay.”

Chanzo: Mwanaspoti